Pata taarifa kuu
TANZANIA-EAC-MSETO-VYOMBO VYA HABARI

Mahakama ya EAC yaruhusu gazeti la Mseto kuendelea na kazi yake

Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki imefuta uamuzi wa kufungwa kwa gazeti la kila wiki la Mseto nchini Tanzania, ambalo lilikua limepigwa marufuku kuchapisha habari yoyote kwa muda wa miaka mitatu tangu Agosti 11, 2016.

Mtu huyu akisoma gazeti la Tanzania huko Arusha, Tanzania, Machi 23, 2017.
Mtu huyu akisoma gazeti la Tanzania huko Arusha, Tanzania, Machi 23, 2017. © AFP
Matangazo ya kibiashara

Gazeti la kila wiki la Mseto lilifungiwa kwa miaka mitatu tarehe 11 Agosti 2016 kwa kosa la "kuchapisha habari za uongo na kuchochea machafuko" baada ya kuchapisha makala inayosema kuwa mshirika wa karibu wa Rais John Pombe Magufuli alikubali kupokea hongo kwa kufadhili kampeni ya rais huyo katika uchaguzi wa mwaka 2015.

Katika uamuzi wake, Mahakama ilibaini kwamba serikali ya Tanzania "haikuonyesha jinsi makala hayo yaliyochapishwa na gazeti la Mseto yalikiukwa maslahi ya umma au kuhatarisha amani na usalama wa raia," kulingana na taarifa iliyotumwa siku ya Alhamisi usiku kwa vyombo vya habari.

Majaji walihitimisha kuwa uamuzi wa kufungwa kwa gazeti hilo uliochukuliwa na wizara ya habari ya Tanzania ulichukuliwa "kwa ukiukwaji mkubwa wa uhuru wa kujieleza," na kuamuru gazeti la Mseto "kuendelea na kazi yake".

Tangu Rais John Magufuli alipochukua hatamu ya uongozi mwishoni mwa mwaka 2015, magazeti kadhaa yamefungwa. Sheria zinazoonekana kama pingamizi kwa uhuru wa kujieleza pia zimepitishwa licha ya maandamano kutoka kwa mashirika ya haki za binadamu.

Tanzania inachukua nafasi ya 93 kwa jumla ya nchi 180, kwenye orodha iliyotolewa mwaka huu 2018 na shirika la Waandishi Wasiokuwa na Mipaka (RSF) (RSF) kuhusu uhuru wa vyombo vya habari. Tanzania imerudi nyuma nafasi 10 ikilinganishwa na mwaka uliopita.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.