Pata taarifa kuu
TANZANIA-UFARANSA-USHIRIKIANO

Ufaransa, Tanzania kufanya mjadala wa kwanza wa kisiasa

Mwezi ujao nchi ya Ufaransa inatarajiwa kuwa na mjadala wa kwanza wa kisiasa utakaowahusisha viongozi wa juu wa Seriali ya Tanzania, lengo likiwa ni kubadilishana uzoefu wa kitaalamu kuhusu ajenda za kimataifa.

Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Frédéric Clavier akizungumza katika studio za RFI Kiswahili, Dar es Salaam. 22/05/2018
Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Frédéric Clavier akizungumza katika studio za RFI Kiswahili, Dar es Salaam. 22/05/2018 RFI Kiswahili
Matangazo ya kibiashara

Akizungumza na idhaa hii katika mahojiano ya kipekee, balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Frederic Clavier, amesema mkutano huu wa kisiasa ni muhimu hasa katika kuimarisha uhusiano wa nchi hizi mbili ambao umekuwa wa kihistoria.

Amesema mkutano huu utakuwa ni fursa ya kipekee ya kubadilishana ujuzi na uzoefu kuhusu masuala ya kimataifa na namna nchi hizo mbili zinaweza kushirikiana katika kujenga dunia salama.

Balozi Clavier ameongeza kuwa kwa kuona umuhimu wa ushirikiano wa kimaendeleo kati ya Tanzania na Ufaransa, nchi yake imeamua kuongeza fedha katika mfuko wa shirika la maendeleo la Ufaransa AFD

"Maendeleo ni kipaumbele kikubwa katika uhusiano wetu, ambapo kupitia shirika letu la maendeleo AFD tumeamua kuongeza mara mbili fedha kutoka euro milioni 50 hadi 100, fedha hizi zitasaidia kwenye huduma za maji, nishati, usafiri lakini pia kilimo".

Akizungumzia kuhusu athari za mabadiliko ya tabia nchi ambazo zimekuwa ni changamoto kidunia na hasa kwa nchi zinazoendelea, balozi Clavier ameipongeza nchi ya Tanzania kwa kutambua umuhimu wa kushughulikia changamoto za kimazingira ikiwa ni pamoja na kuridhia mkataba wa Paris kuhusu mazingira.

"Mabadiliko ya tabia nchi ni suala mtambuka ambalo tunapaswa kukabiliana nalo sote kwa pamoja, kwa hivyo ni muhimu kuona Tanzania inashiriki na tunakaribisha uamuzi wa Serikali kufanyia kazi suala hili na nikutokana na ukweli kuwa tanzania inao uwezo mkubwa hasa kwenye masuala ya nishati".

Katika hatua nyingine balozi Clavier amezungumzia umuhimu wa vyombo vya habari katika kuchangia maendeleo ya nchi, ambapo amesema Serikali ya Ufaransa itaendelea kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wa habari katika kubadilisha uzoefu na taarifa ambazo zitaendelea kuimarisha uhusiano wa nchi hizi mbili.

Balozi Clavier amesema haya wakati alipotembelea studio za idhaa ya Kiswahili ya Radio France International inayotangaza kutoka Dar es Salaam, Tanzania.

Hivi karibuni ujumbe wa wafanyabiashara zaidi ya 35 kutoka nchini Ufaransa ulitembelea nchini ya Tanzania ambapo walikutana na wadau wa sekta binafsi pamoja na viongozi wa Serikali.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.