Pata taarifa kuu
BURUNDI-SIASA-USALAMA

Wapiga kura kuelekea kura ya maoni waanza kuandikwa Burundi

Tume ya uchaguzi nchini Burundi CENI imeanza kusajili wapiga kura watakaoshiriki katika kura ya maoni iliyopangwa kufanyika mwezi Mei mwaka huu, kura ambayo inapingwa vikali na vyama vya upinzani.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi nchini Burundi (Céni) Pierre Claver Ndayicariye
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi nchini Burundi (Céni) Pierre Claver Ndayicariye AFP PHOTO / LANDRY NSHIMIYE
Matangazo ya kibiashara

Mwenyekiti wa tume hiyo Pierre-Claver Ndayicariye amesema zoezi hilo litafanyika nchi nzima na kutakuwa na vituo ambavyo wananchi watatakiwa kujitokeza kila siku hadi tarehe 17 ya mwezi huu.

Zoezi hili hata hivyo limekosolewa vikali na upinzani wanaosema ni njama ya kuhakikisha mabadiliko ya katiba yanafanyika kutoa nafasi kwa rais Pierre Nkurunziza kuendelea kusalia madarakani.

Mapema wiki hiii Katibu mkuu wa umoja wa Mataifa Antonio Guterres alikosoa jaribio la rais wa Burundi Pierre Nkurunziza kutaka kubadilisha katiba ya nchi hiyo hatua ambayo itamruhusu kukaa madarakani kwa muongo mwingine au zaidi.

Katibu mkuu Guterres alisema upinzani na mashirika ya kiraia ni lazima yashirikishwe kwenye maamuzi yoyote ya kubadili katiba ili kuzuia uwezekano wa nchi hiyo kutumbukia kwenye mzozo zaidi.

Guterres aliongeza kuwa anatambua Burundi kama nchi inayo mamlaka ya kujiamulia mambo yake kama taifa huru lakini akaonya kuwa jambo la kubadili katiba linahitaji maridhiano ya pande zote.

Tume ya uchaguzi nchini Burundi Ceni inasema usajili huu pia utatumika katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.