Pata taarifa kuu
TANZANIA-UPINZANI

Tundu Lissu:Shambulio dhidi yangu lilikuwa ni mauaji ya kisiasa

Mbunge wa upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu amesema shambulio dhidi yake lililotokea Septemba saba mwaka 2017 lilikuwa sawa na mauaji ya kisiasa.

Mwanasiasa wa upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu, akizungumza na Wanahabari katika hosoitali ya Nairobi nchini Kenya Januari 05 2018
Mwanasiasa wa upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu, akizungumza na Wanahabari katika hosoitali ya Nairobi nchini Kenya Januari 05 2018 www.mwananchi.co.tz
Matangazo ya kibiashara

Lissu ambaye pia ni mnadhimu mkuu wa upinzani alishambuliwa na watu wasiojulikana akiwa nje ya makazi yake Mkoani Dodoma, nchini Tanzania baada ya kuhudhuria kikao cha bunge.

Tangu hapo mbunge huyo machachari amekuwa akipatiwa matibabu katika hospitali ya Nairobi nchini Kenya.

Kiongozi huyo amezungumza kwa mara ya kwanza na vyombo vya habari nchini Kenya, tukio lilivuta hisia za mamilioni ya watanzania waliokuwa wakifuatilia kupitia mitandao ya kijamii.

“Mimi sio mfanyabiashara na nimeshambuliwa katika eneo wanaloishi viongozi wa bunge na ambalo lina ulinzi, kwa maoni yangu shambulio hilo ni sawa na mauaji ya kisiasa,”amesema mbunge huyo na kueleza kuwa alimiminiwa risasi 16 kwenye mwili wake.

Baada ya kukamilisha hatua ya kwanza ya matibabu, Mbunge huyo ambaye pia ni rais wa Mawakili wa Tanganyika, anatarajiwa kwenda Ulaya kwa matibabu zaidi.

Serikali ya Tanzania imekuwa ikisema kuwa, inaendelea na uchunguzi kubaini waliomshambulia mwanasiasa huyo wa upinzani.

Msemaji wa serikali Dokta Hassan Abbasi, amesema serikali haiwezi kumjibu Lissu kwa sasa.

"Mhe Lissu bado ni mgonjwa na yuko wodini hivyo Serikali haioni busara kulumbana naye kwa sasa. Tunaendelea kumuombea apone haraka," ameandika katika ukurasa wake wa Twitter.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.