Pata taarifa kuu
RWANDA

Kuna hofu ya kuzuka baa la njaa kaskazini mwa nchi ya Rwanda

Wasiwasi umeanza kutanda miongoni mwa wakazi wa Nyagatare wakihofia kukumbwa na baa la njaa na hofu hiyo imejiri baada ya kukosekana kwa mvua ya kutosha katika baadhi ya maeneo ya kaskazini mashariki ya Rwanda.

Zaidi ya watu milioni 14 kukabiliwa na njaa Kusini mwa Bara la Afrika kutokana na ukame
Zaidi ya watu milioni 14 kukabiliwa na njaa Kusini mwa Bara la Afrika kutokana na ukame WFP via twitter
Matangazo ya kibiashara

Tayari baadhi ya mimea mashambani imeanza kunyauka kutokana na jua kali.

Tarafa za Rukomo na Tabagwe ni miongoni mwa maeneo ya kaskazini mashariki ya Rwanda yaliyoathiriwa na ukame kwa kiasi kikubwa, wakulima katika maeneo hayo hawana matumaini yoyote ya kuvuna kile walichopanda kwani kadri siku zinavyosonga mbele ndivyo mazao yao yanavyozidi kukauka.

“Hatuna matumaini ya kuvuna msimu huu, jua ni kali sana mazao yetu yameanza kukauka, waliopanda mbegu mwanzoni hawakufanikiwa na sisi tumejaribu lakini jua limeharibu mazao yetu”.

“Mahindi yote yamekauka, hakuna mtu hata mmoja atakayeambulia kitu msimu huu”.

Wakazi hao wameshindwa kukanusha kuwa njaa haipo miongoni mwao.

“Kusema kweli watu tuna njaa, hata hao wafanyabiashara waliokuwa wameweka akiba ili watuuzie, na wao wameishiwa, hatujui tutaishije”.

Hata hivyo wataalamu wa kilimo katika maeneo hayo wameanzisha kampeni ya kuwatowa wasiwasi wakazi ambao mashamba yao yamekubwa na ukame, na wanadai kuwa, eneo kubwa la kilimo kaskazini mashariki mwa Rwanda limeshuhudia mvua, hivyo wakazi katika eneo la Nyagatare, wasihofu kukumbwa na baa la njaa kama ilivyotokea mwaka jana. Hayo ni kwa mujibu wa Rutayisire Gilbert afisa ugani wilayani Nyagatare.

“Maeneo ambayo yamekumbwa na ukame siyo mengi, maeneo makubwa yamepata mvua ya kutosha na mpaka sasa tunavyoongea, watu wanaoishi pembezoni mwa mito tumeanza kuwasaidia namna wanaweza kumwagilia mazao yao kwa kutumia mitambo”.

Miaka ya hivi karibuni watu kadhaa wameripotiwa kuhama makazi yao, kuelekea Tanzania na Uganda kwa kile ambacho kimedaiwa walikimbia njaa iliyoyakumba baadhi ya maeneo ya Rwanda.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.