Pata taarifa kuu
KENYA-SIASA-UCHAGUZI

Wafula Chebukati: Nawapa wanasiasa kadi ya njano, Tume ya Uchaguzi imegawanyika

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi nchini Kenya Wafula Chebukati amesema hatajiuzulu hata baada ya mmoja wa Makamishena wa Tume hiyo Roselyn Akombe kutangaza kujiuzulu mapema hivi leo.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi nchini Kenya Wafula Chebukati
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi nchini Kenya Wafula Chebukati IEBCKenya
Matangazo ya kibiashara

Chebukati amekiri kuwa kuna mgawanyiko ndani ya Tume hiyo na maelekezo yake kama ya kisheria wakili na Mwenyekiti, yamekuwa hayaungwi mkono na Makamishena ndani ya Tume hiyo.

“Sina uhakika iwapo Uchaguzi utakuwa huru na haki, na iwapo nitakuwa Mwenyekiti wa Tume hii katika mazingira haya,” amesema.

"Nawaomba Watumishi ndani ya Tume ya Uchaguzi waliotajwa wajiuzulu, sitaki jina langu kuharibiwa katika Uchaguzi huu,".

Pamoja na hilo, Chebukati amesema amejitahidi kuhakikisha kuwa Uchaguzi wa tarehe 26 unafanyika katika mazingira magumu lakini inavyoonekana ni ngumu.

Aidha, amesema anawapa kadi ya njano wanasiasa nchini humo na kuwataka kuacha kuwatisha Makamishena na wafanyikazi wa Tume hiyo, ili watekeleze majukumu yao ipasavyo.

“Nilipewa kazi hii, kuhakikisha kuwa naitumikia nchi yangu na kuhakikisha kuwa Uchaguzi unafanikiwa na hili nitahakikisha kuwa linafanyika,” alisema Chebukati.

“Kujiuzulu lingekuwa jambo rahisi sana kufanya hivyo kwangu hasa kipindi hiki lakini sitajiuzulu,” aliongeza.

Mgawanyiko ndani ya Tume ya Uchaguzi, umezua wasiwasi iwapo usimamizi huo utakuwa huru na haki.

Rais Uhuru Kenyatta mapema siku ya Jumatano, alitangaza kuwepo kwa maombi ya kitaifa nchini humo na kusisitiza kuwa ni lazima Uchaguzi huo unafanyika wiki ijayo.

Hata hivyo, kiongozi wa muungano wa upinzani NASA Raila Odinga, amesema hatashiriki katika Uchaguzi huo iwapo mabadiliko hayatafanyika.

 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.