Pata taarifa kuu
KENYA-MAANDAMANO-UCHAGUZI

NASA yafuta maandamano ya Jumanne hii Kenya

Muungano wa upinzani nchini Kenya NASA, umeahirisha maandamano ya leo Jumanne kote nchini ili viongozi kuwatembelea wafuasi wao waliojeruhiwa na kutembelea familia zilizopoteza wapendwa wao baada ya kupigwa risasi na Polisi.

Kiongozi wa muungano wa upinzani nchini kenya, Raila Odinga.
Kiongozi wa muungano wa upinzani nchini kenya, Raila Odinga. REUTERS/Thomas Mukoya
Matangazo ya kibiashara

Kiongozi wa muungano wa upinzani NASA, Raila Odinga ,amesema atawaongoza viongozi wenzake kuwatembelea waandamanaji waliothirika kabla ya maandamano ya kila wiki kurejelewa kesho.

Wanasiasa wa upinzani wameendelea kulishutumu jeshi la polisi kwa kutumia nguvu kupita kiasi kukabiliana na wafuasi wao wakati wa maandamano hayo, yanayolenga kushinikiza mabadiliko ndani ya Tume ya Uchaguzi kuelekea Uchaguzi mpya wa urais tarehe 26 mwezi huu.

Siku ya Jumatatu, mwanafunzi wa kidato cha nne, alipigwa risasi na kupoteza maisha mjini Kisumu Magharibi mwa nchi hiyo wakati wa maandamano hayo.

Polisi kwa upande wake, imekanusha madai hayo na kujitetea kuwa inatekeleza agizo la serikali iliyopiga maarufu maandamano katikati ya miji ya Kisumu, Nairobi na Mombasa.

Tuhma dhidi ya polisi zimeendelea kutolewa, baada ya kutolewa kwa ripoti ya mashirika mawili ya kutetea haki za Binadamu, Amnesty International na Human Rights Watch ambayo yamelishtumu jeshi hilo kwa kuwauwa wafuasi wa upinzani zaidi ya 30 kwa kuwapiga risasi tangu mwezi Agosti.

Wakati huo huo, licha ya Waangalizi wa Umoja wa Ulaya kusema wameanza kuridhika na hatua zinazochukuliwa na Tume ya Uchaguzi kufanikisha Uchaguzi huo, wametoa wito wa mazungumzo kati ya Odinga na rais Uhuru Kenyatta.

Odinga tayari amejiondoa kwenye Uchaguzi huo, na kuna hofu kuwa huenda akawaambia wafuasi wake wasipige kura.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.