Pata taarifa kuu
KENYA-SIASA-UCHAGUZI

Wakenya wasubiri matokeo ya urais kwa wasiwasi

Hali ya wasiwasi inaendelea kushuhudiwa katika ngome za upinzani nchini Kenya wakati huu Tume ya Uchaguzi inapoendelea kupitia upya matokeo ya urais katika ukumbi wa Bomas of Kenya jijini Nairobi.

Kura zilivyohesabiwa
Kura zilivyohesabiwa REUTERS/Thomas Mukoya
Matangazo ya kibiashara

Kufikia siku ya Alhamisi asubuhi, Kamishena wa tume hiyo Roselyn Akombe alidokeza kuwa zoezi hilo linakwenda vizuri na mawakala kutoka muungano wa upinzani NASA na JUBILEE wanapitia fomu maalum kutoka maeneo bunge na vituo vya kujumuisha matokeo aina ya 34 A na 34 B.

Kamishena wa Tume hiyo Bi. Roselyn Akombe ameomba wakenya kuwa watulivu na wavumilivu kipindi hiki, kura zinapoendelea kupitiwa upya.

“Tunaendelea vizuri katika zoezi hili, tunaomba uvumilivu wao ili tulimalize vema,” amesema Bi. Akombe.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo Ezra Chiloba amekanusha madai ya muungano wa NASA kuwa mfumo wa ukusanyaji wa matokeo umedukuliwa na kubadili matokeo.

Kauli hii imezua wasiwasi miongoni mwa wadau wanaofuatilia upitiaji wa matokeo hayo, baada ya Mwenyekiti wa Tume Wafula Chebukati kusema kuwa walikuwa wanachunguza madai hayo.

Waangalizi wa Uchaguzi huo, Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya na wengine akiwemo aliyekuwa Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry anayewakilisha taasisi ya Jimmy Carter, wanatarajiwa kutoa mtazamo wao kuhusu Uchaguzi Mkuu nchini humo uliofanyika siku ya Jumanne.

Waangalizi wa Uchaguzi kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki wamewataka wakenya kuwa watulivu kipindi hiki matokeo yanapopitiwa upya.

Jijini Nairobi, wasiwasi umeendelea kushuhudiwa huku shughuli za kawaida zikirejea polepole, hata hivyo, maduka yamefungwa na watu wana hofu ya kurejea kazini.

Hali hii inashuhudiwa katika maeneo mbalimbali nchini humo kama Mombasa na Kisumu, Magharibi mwa nchi hiyo.

Hata hivyo, watu wanne wamepoteza maisha baada ya kupigwa risasi na polisi katika mtaa wa Mathare jijini Nairobi.

Ripoti hizi zimejiri, baada ya wafuasi wa muungano NASA, kulalamika kuwa kumekuwa na wizi wa kura.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.