Pata taarifa kuu
KENYA-UCHAGUZI

IEBC yakanusha kudukuliwa kwa mfumo wa kukusanya matokeo ya uchaguzi Kenya

Tume ya uchaguzi nchini Kenya IEBC imetupilia mbali madai ya muungano wa upinzani nchini humo NASA, ambao siku ya Jumatano ulitoa madai kuwa mfumo wa ukusanyaji matokeo wa IEBC ulidukuliwa kubadili matokeo.

Maandamano ya wafuasi wa Raila Odinga katika eneo la Kondele, Agosti 9, 2017.
Maandamano ya wafuasi wa Raila Odinga katika eneo la Kondele, Agosti 9, 2017. FREDRIK LERNERYD / AFP
Matangazo ya kibiashara

Akiongea na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Bomas of Kenya ambao ndio kituo kikuu cha tume ya uchaguzi IEBC kutangazia matokeo, afisa mkuu wa uchaguzi Ezra Chiloba ametupilia mbali madai ya upinzani yaliyotolewa na vinara wake hapo siku ya Jumatano.

Chiloba amesema kuwa mfumo unaotumiwa na IEBC kukusanya matokeo na kuyatangaza haukudukuliwa kama ilivyodaiwa na upinzani na kwamba baada ya uchunguzi wao wa ndani wamejiridhisha kuwa mfumo wao haukuingiliwa wakati wowote.

Siku ya Jumatano, akizungumza na waandishi wa habari kwenye Hotel ya Carrabel, kinara wa upinzani Raila Odinga alidai kuwa timu ya wataalamu wake wa mtandao walibaini kuwepo kwa udanganyifu.

Kwa sasa IEBC inasema imeshapokea matokeo kutoka kwenye vituo vyote vya uchaguzi kwa zaidi ya asilimia 96 na kwamba ni vituo vichache tu ndio vimesalia.

Kwa majibu haya ni wazi sasa tume ya uchaguzi IEBC itaendelea na kazi yake huku kitendawili kikiwa ni je hatua gani kutoka sasa muungano wa upinzani NASA itachukua kupaza sauti yake?

Katika hatua nyingine hapo jana kulishuhudiwa makabiliano kati ya polisi na waandamanaji kwenye mtaa wa Huruma mjini Mathare ambapo kundi la vijana waliokuwa na silaha walikuwa wakishinikiza matokeo rasmi kutangazwa.

Kinachosubiriwa sasa ni matokeo ya mwisho kujua mbivu na mbichi za kinyang’anyiro hichi, ambapo kwa mujibu wa sheria tume ya IEBC inapaswa kumtangaza mshindi wa kiti cha urais ndani ya siku 7 baada ya kupiga kura.

Tayari rais anaye maliza muda wake Uhuru Kenyatta anaongoza kwa kura 54%, huku mpinzani wake Raila Odinga akipata kura 44%.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.