Pata taarifa kuu
KENYA-SIASA-UCHAGUZI

Kenya: Vifaa vya kupigia kura vyawasili katika vituo vya kupigia kura

Tume ya Uchaguzi nchini Kenya inasema iko tayari kusimamia Uchaguzi Mkuu utakaofanyika hapo kesho.

Vifaa vya kuoigia kura nchini Kenya
Vifaa vya kuoigia kura nchini Kenya Reuters/Baz Ratner
Matangazo ya kibiashara

Maafisa wa Tume ya Uchaguzi wamekuwa wakipokea vifaa vya kupigia kura, ikiwemo masanduku na karatasi za kupigia kura.

Kampeni zilimalizika  Jumamosi iliyopita huku ushindani mkubwa wa urais ukiwa ni kati ya rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga. Wote wamesema wana imani kuwa watashinda Uchaguzi huu.

Rais Kenyatta atapiga kura katika eneo bunge la Gatundu katika Kaunti ya Kiambu huku Odinga akipiga kura yake katika Shule ya Msingi ya Olympics, katika mtaa wa Kibera jijini Nairobi.

Wakenya zaidi ya Milioni  19, wanatarajiwa kushiriki katika Uchaguzi huo kutoka Kaunti zote 47 nchini humo na mbali na urais, watachaguwa Magavana, Maseneta, Wabunge, Wawakilishi wa Wanawake na wawakilishi wa serikali za Kaunti.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Wafula Chebukati, amewahakikishia Wakenya kuwa wao kama Tume wameweka mikakati yote tayari kuhakikisha kuwa zoezi hili linakwenda vizuri na Uchaguzi unakuwa huru na haki.

Aidha, amesema kuwa wakenya wasiwe na wasiwasi  kuhusu urushaji na kutangazwa kwa matokeo kwa sababu ni suala ambalo limeshughulikiwa ipasavyo.

Kumekuwa na Wakenya wengi wanaosafiri vijijini, kwa kile wanachosema wanakwenda kupiga kura.

Hata hivyo, kumekuwa na mashaka kuwa wengine wamerudi vijijini kwa sababu wanahofia kuwa huenda kukazuka machafuko kama ilivyokuwa baada ya Uchaguzi wa mwaka 2007.

Wito umekuwa ukitolewa kwa wananchi wa taifa hilo, kudumisha amani kabla na baada ya uchaguzi.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.