Pata taarifa kuu
KENYA-SIASA-UCHAGUZI

IEBC:Tuko tayari kuandaa Uchaguzi Mkuu nchini Kenya

Tume ya Uchaguzi nchini Kenya inasema iko tayari kuandaa Uchaguzi wa tarehe nane mwezi ujao.

Afisa wa Tume ya Uchaguzi nchini Kenya
Afisa wa Tume ya Uchaguzi nchini Kenya REUTERS/Thomas Mukoya
Matangazo ya kibiashara

Mwenyekiti wa Tume hiyo Wafula Chebukati akilihotubia taifa jijini Nairobi, amesema kila kitu kinakwenda kama ilivyopangwa na hakuna mashaka kuwa zoezi hili litakwenda vizuri.

Aidha, amesema kuwa yeye na Makamishena wenzake wamefanya bidii na kufanya maandalizi ya kutosha kuhakikisha kuwa zoezi hilo litakuwa huru na haki na kila mmoja kuyakubali matokeo.

“Sisi kwa upande wetu, tumefanya tuwezalo kuhakikisha kuwa Uchaguzi huu unakwenda vizuri,” amesema Chebukati.

“Kazi inayosalia ni kwa Wakenya kujitokeza kwa wingi na kupiga kura ili kuwachagua viongozi wao,” ameongeza.

Katika hatua nyingine, Tume hiyo ya Uchaguzi, imesema imeweka mikakati kuhakikisha kuwa, mfumo wa eletroniki unafanya kazi katika vituo vyote vya kupigia kura ili kuweka uwazi katika zoezi hilo.

Tume hiyo imekariri kuwa, wakenya kwa mara ya kwanza watapata nafasi ya kufahamu matokeo hata kabla ya kufika katika makao makuu ya kuyajumuisha jijini Nairobi.

Hii inatokana na sheria kuwataka wasimamizi wa Uchaguzi katika majimbo yote 290, kutangaza matokeo ya urais na kubandika ili wananchi wayafahamu.

Vyombo vya Habari na vyama vya siasa navyo vitakuwa na fursa ya kuyafahamu matokeo na kuyajumuisha lakini, tume ndio itakayokuwa ya mwisho kumtangaza mshindi wa kiti cha urais.

Kwa mara ya kwanza, matokeo ya urais hayatangazwa hatua kwa hatua kama ilivyokuwa miaka iliyopita, bali Tume ya Uchaguzi itakuwa na kazi ya kujumuisha matokeo hayo na kumtangaza mshindi wa urais.

Katiba ya Kenya inaeleza kuwa mshindi anastahili kupata asilimia 50 ya kura zote zilizopigwa kote nchini na asilimia 25 katika Kaunti 24 kati ya 47 nchini humo.

Ikiwa hakutakuwa na mshindi katika mzunguko wa kwanza, kutakua na duru ya pili kati ya aliyeibuka wa kwanza na yule wa pili.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.