Pata taarifa kuu
DUNIA-WAFANYIKAZI

Wafanyakazi duniani wadai nyongeza ya mshahara na kuthaminiwa

Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati yameugana na mataifa mengine duniani kuadhimisha sikukuu ya Wafanyikazi duniani siku ya Jumatatu.

Waandamanaji jijini Paris nchini Ufaransa wakati wa maadhimisho ya siku ya wafanyikazi Mei 1 2017
Waandamanaji jijini Paris nchini Ufaransa wakati wa maadhimisho ya siku ya wafanyikazi Mei 1 2017 Reuters
Matangazo ya kibiashara

Haya ni maadhimisho ya kila mwaka na siku kama ya leo, wafanyikazi duniani hutumia kudai nyongeza ya mshahara na kutaka kuthaminiwa na waajiri wao.

Kutokana na kupanda kwa gharama ya maisha, wafanyikazi wamekuwa wakishinikiza nyongeza ya mshahara kutoka kwa waajiri wao ili kumudu hali ngumu ya kiuchumi inayowakabili.

Serikali na waajiri wengine wametumai siku hii, kuendelea kutoa ahadi ya kulinda haki za wafanyikazi, lakini pia kuwahakikishia kuwaboreshea mazingira ya kufanya kazi.

Vyama vya wafanyikazi kote duniani na hata barani Afrika mfano wa COSATU nchini Afrika Kusini na COTU nchini Kenya, vimekuwa na ushawishi wa kisiasa kutokana na kuwa na idadi kubwa ya wanachama.

Nchini Kenya, maadhimisho ya mwaka huu yaliongozwa na rais Uhuru Kenyatta ambaye alitumia siku hiyo kuhimiza uchaguzi wa amani mwezi Agosti mwaka huu.

Aidha, ametangaza kuwa mshahara wa wafanyikazi nchini humo umeongezwa kwa asilimia 18, kuanzia mfanyikazi anayepata mshahara wa chini wa Dola 130 kwa mwezi.

Kiongozi huyo pia ameelezea mafaniko ya serikali yake kwa muda miaka minne iliyopita, ikiwa ni pamoja na kufufua viwanda vilivyounda nafasi zaidi za kazi.

"Tunawaomba mtupigie kura ili tuendelee na kazi hii nzuri," alisema rais Kenyatta.

Nchini Tanzania rais John Magufuli naye, amesema wafanyikazi nchini humo wameamua kufanya kazi kwa bidii ili kufikia malengo ya kufikia uchumi wa viwanda nchini humo.

Aidha, ameeleza kuwa madai ya wafanyikazi nchini humo ikiwa ni pamoja na mifuko ya hifadhi ya jamii kuwalipa fedha zao ikiwa watapoteza kazi kabla ya kuustafu, linashughulikiwa na serikali yake.

Kuhusu nyongeza ya mshahara, rais huyo amesema kuwa hawezi kuongeza mshahara kwa wafanyikazi hadi pale changamoto za wafanyikazi hewa litakapotatuliwa kwanza.

Hata hivyo, Magufuli ametangaza kuwa serikali yake itawaajiri wafanyikazi wapya 52,000 mwaka huu.

Nchini Uganda, rais Yoweri Museveni amewataka wafanyikazi nchini humo kuijenga Uganda kupitia sera nzuri.

Nchini Ugiriki maelfu ya wafanyikazi wameandamana jijini Athens na kutangaza mgomo wa siku nzima, kushinikiza serikali kuimarisha uchumi wa nchi hiyo.

Serikali ya Ugiriki imepanga kupunguza kazi na mishahara katika sekta ya  umma tarehe 17 mwezi huu.

Nchini Ufaransa, kumekuwa na maandamano makubwa katika miji mbalimbali nchini humo kuishinikiza serikali kuboresha maslahi ya wafanyikazi.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.