Pata taarifa kuu
TANZANIA-UFARANSA

Tanzania: Serikali ya sasa haina urasimu kwa wawekezaji

Serikali ya Tanzania kupitia vizara ya viwandam biashara na uwekezaji, imewatoa hofu wawekezaji wa kigeni ambapo imewataka waende kuwekeza kwa uwingi nchini humo kwa kuwa mazingira ya sasa yanaruhusu.

Katibu mkuu wizara ya viwanda, biashara na uwekezaji nchini Tanzania, Profesa Adolf Mkenda.
Katibu mkuu wizara ya viwanda, biashara na uwekezaji nchini Tanzania, Profesa Adolf Mkenda. DP
Matangazo ya kibiashara

Katibu mkuu wa wizara hiyo Profesa Adolf Mkenda, ambaye alimuwakilisha waziri wa viwanda Charles Mwijage, amesema kwa sasa hakuna urasimu kwenye ofisi nyingi za uma na kwamba wamejitahidi kuanzisha vituo maalumu vya msaada wa wawekezaji kwenye kituo cha uwekezaji nchini Tanzania.

Kwenye mahojiano ya kipekee na mwandishi wa idhaa ya rfikiswahili, Profesa Mkenda amesema Serikali ya awamu ya tano imeshaapa kuhakikisha inawavutia wawekezaji wengi kadiri inavyowekana hatua ambazo zinaenda sambamba na uboreshwaji wa mazingira ya uwekezaji.

Kuhusu hofu waliyokuwanayo wawekezaji kutoka nje, katibu mkuu Mkenda anasema nia ya rais John Magufuli ni kuhakikisha wizara zinazohusika zinawahudumia ipasavyo wawekezaji na ndio maana hata wakati alipoingia madarakani alifanya mkutano na wafanyabiashara kutoka sekta binafsi.

“Ushahidi upo kuwa sasa hakuna urasimu, kama unakumbuka rais Magufuli alipoingia madarakani, mkutano wake wa kwanza ulikuwa ni kati yake na wafanyabiashara kutoka sekta binafsi, hii inaonesha nia njema aliyonayo rais kuhakikisha Serikali inafanya kazi kwa ukaribu na wawekezaji wa ndani na wale wa nje.” alisema Mkenda.

Akitoa mada wakati wa mkutano wa jukwaa la kibiashara kati ya Ufaransa na Tanzania, katibu mkuu Mkenda amesema Serikali inalenga kupata wawekezaji watakokuja nchini na kuanzisha viwanda ambavyo vitaendana na hali halisi, akitoa mfano kama kiwanda cha ngozi ambazo kitatoa fursa kwa wafugaji au kiwanda cha bidhaa za kilimo ambacho kitatoa fursa kwa wakulima wa Tanzania.

Mkenda amesema maeneo ambayo nchik imelenga sana kwa uwekezaji ni pamoja na kwenye nishati, miundombinu, sayansi na teknolojia pamoja na utalii ambao amesema nchi ya Ufaransa ni maarufu duniani kwa kutembelewa na watalii wengi.

Kwa upande wa makampuni ya Ufaransa yanayojihusisha na nishatim gesi na mafuta, yamesema baadhi yao tayari wameanza kazi nchini Tanzania na kwenye nchi nyingine za ukanda na tayari wamevutiwa na hali inayoonekana kwa sasa.

Kampuni ya Total ambayo itajenga bomba la mafuta kutoka nchini Uganda hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania, inasema licha ya changamoto za ujenzi wa bomba hilo, lakini imeridhishwa na namna Serikali hizi mbili zilivyojitolea kuhakikisha malengo ya ukuaji wa uchumi wao kupitia mafuta na gesi yanatimia.

Kwa upande wa makampuni ya Bouygues, Engie, GE na Siemens France, yote kwa pamoja yamekiri kuwa tayari wameingia mikataba kadhaa na Serikali ya Tanzania kwenye sekta ya nishati na wanatarajia kupanua wigo zaidi wa kutoa huduma hiyo kwa Tanzania.

Wafanyabiashara na wadau zaidi ya 200 waliosafiri na kuja Tanzania kushiriki mkutano huu, wameonesha kuridhishwa na matokeo ya mkutano wenyewe ambapo hawakusita kuimwagia sifa Serikali ya Tanzania pamoja na nchi wanachama za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.