Pata taarifa kuu
KENYA-TANZANIA

Mahakama nchini Kenya yasitisha kwa muda mchakato wa kuwaajiri Madaktari kutoka Tanzania

Mahakama Kuu inayoshughulikia maswala ya ajira nchini Kenya imesitisha kwa muda hatua ya serikali nchini humo kuwaajiri Madaktari kutoka nchini jirani ya Tanzania.

Madaktari nchini Kenya wakiwa na mabango kushinikiza kusikilizwa wakati walipoandamana hivi karibuni jijini Nairobi.
Madaktari nchini Kenya wakiwa na mabango kushinikiza kusikilizwa wakati walipoandamana hivi karibuni jijini Nairobi. REUTERS/Thomas Mukoya
Matangazo ya kibiashara

Jaji Nelson Abuodha ameagiza mchakato huo kusitishwa hadi pale kesi ya Madaktari hao itakaposikilizwa na uamuzi kutolewa.

Kesi hiyo imewasilishwa na Madaktari watano wanaotaka serikali ya Kenya kuwaajiri Madaktari 1400 ambao hawana kazi nchini humo kabla ya kuamua kuwaajiri 500 kutoka nchini Tanzania.

Mahakama hiyo imewataka Madaktari hao kutoa taarifa ya kesi hiyo kwa Wizara ya afya kwa muda wa siku 21.

Kesi hiyo itatajwa tarehe 19 mwezi Aprili.

Tayari serikali ya Tanzania imekubali kuwa Madaktari wake 500 ambao hawajaajiriwa wapewe ajira nchini Kenya na wiki hii Wizara ya afya nchini humo imesema kuwa tayari Madaktari 400 wamewasilisha maombi ya kwenda kufanya kazi nchini Kenya.

Kenya ilikwenda kuwatafuta Madaktari nje ya nchi wakati Madaktari wake walipokuwa wanagoma kudai nyongeza ya mshahara na kutaka serikali kuimarisha mazingira ya utendea kazi.

Mgomo wa Madaktari nchini Kenya ulidumu kwa siku 100 kabla ya kumalizika.
 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.