Pata taarifa kuu
TANZANIA-KENYA-AFYA

Madaktari wa Tanzania wakataa kutumikia Kenya

Chama cha Madaktari nchini Tanzania kimefutilia mbali mpango wa kuwatuma madaktari 500 nchini Kenya wakisema Tanzania ina upungufu mkubwa wa madaktari.

Mmoja wa madaktari ambao walihiriki mgomo, wakiandamana hivi karibuni jijini Nairobi.
Mmoja wa madaktari ambao walihiriki mgomo, wakiandamana hivi karibuni jijini Nairobi. REUTERS/Thomas Mukoya
Matangazo ya kibiashara

Hivi karibuni nchi ya Tanzania ilikubali ombi la kuipatia Kenya madaktari 500 watakaoisaidia nchi hiyo kukabiliana na tatizo la uhaba wa madaktari katika vituo vyake vya tiba hasa baada ya kutokea kwa mgomo wa madaktari nchini humo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli alikubali kutoa madaktari hao, baada ya kufanya mazungumzo na ujumbe wa viongozi wa Wizara ya Afya kutoka Kenya uliotumwa na Rais wa nchi hiyo Uhuru Kenyatta.

Kenya imeshuhudia mgomo wa madaktari uliomalizika wiki jana baada ya mgomo huo kudumu kwa siku 100.

Miongoni mwa mengine, maafisa wa MAT wamesema wanahitaji ufafanuzi kuhusu ni kwa nini Serikali ya Kenya imeshindwa kuajiri Madaktari wake na kuanza kutafuta Madaktari kutoka Tanzania huku ikizingatiwa kwamba malipo ya Madaktari wa Tanzania yatakuwa makubwa zaidi ya wenyeji.

Chama cha Madaktari nchini Tanzania pia kinataka kujua ni kwa jinsi gani Madaktari wataweza kufanya kazi bila kukamilisha taratibu za kisheria kama vile kufanya mitihani ya Bodi na kusajiliwa ili kupata uhalali wa kutibu.

"MAT inasisitiza kwamba ni muhimu kusitisha zoezi la kuwapeleka Madaktari wa Tanzania mpaka hapo Serikali ya Kenya itakapoanza utekelezaji wa makubaliano kati yake na Madaktari wao," chama hicho kimesema.

Serikali ya Kenya imetetea hatua yake ya kutoa nafasi za ajira kwa madakatari kutoka nchi za nje kuboresha sekta ya afya. Hii ni baada ya muungano wa madaktari KMPDU, kuishtumu serikali kwa kufanya uamuzi huo na kuwapuuza matatabibu wake wasio na ajira.

Wakati huo huo Waziri wa Afya nchini Kenya Cleopha Mailu amewatembelea wagonjwa katika hospitali ya taifa ya Kenyatta jijini Nairobi na kuzungumza na Madakatari baada ya kumaliza mgomo wao wa siku 100 wiki iliyopita.

Mbali na ziara hiyo, Waziri huyo amesema kuwa Madaktari 500 watakaoajiriwa kutoka Tanzania, wanatarajiwa kuwasili nchii humo hivi karibuni ili kusaidia kutoa huduma hiyo katika kaunti mbalimbali.

Amekanusha madai kutoka chama cha Madaktari nchini humo kuwa serikali imekataa kuwaajiri Madaktari kutoka nchini humo, na kusisisitiza kuwa wamekataa ajira wenyewe.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.