Pata taarifa kuu
UGANDA-SIASA-USALAMA

Mzozo katika Ufalme wa Rwenzururu unahitaji suluhu ya kisiasa

Ufalme wa Rwenzururu, unapatikana katika jimbo la Rwenzori Kusini Magharibi mwa Uganda karibu na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Eneo la  Rwenzururu,  nchini Uganda
Eneo la Rwenzururu, nchini Uganda Wikimedia
Matangazo ya kibiashara

Watu wanaoishi katika jimbo hilo ni kutoka makabila ya Bakonzo, Banande, Bamba na Basumba wanaoishi karibu na Milima ya Rwenzori.

Charles Wesley Mumbere ndio Mfalme wa sasa wa eneo hilo la Rwenzururu na anafahamika kwa jina maarufu kama Omusinga.

Alipewa cheo cha Ufalme akiwa na umri wa miaka 13 baada ya kifo cha baba yake, na kuanza kuwa Mfalme rasmi akiwa na umri wa miaka 18, mwaka 1966.

Ufalme huo ulianzishwa mwaka 1962, baada ya watu wa Bakonzo kuunda vuguvugu la kutaka kujitenga na nchi ya Uganda.

Mapambano hayo ambayo hayajawahi kuzaa matunda yaliyoongozwa na baba wa Mfalme wa sasa Mukirania Kibanzang.

Serikali na Ufalme wa Rwenzururu
Mwaka 2005, rais Yoweri Museveni aliunda Kamati maalum kuangalia maswala ya muda mrefu yaliyokuwa yanaikumba Ufalme huo.

Baada ya uchunguzi huo serikali ilibainika kuwa asilimia 90 ya watu wa kabila la Bakonzo wanaunga mkono Ufalme huo unaoongozwa na Mfalme Mumbere.

Kutokana na matokeo ya uchunguzi huo, mwaka 2009, serikali ya rais Museveni ilitambua rasmi Ufalme huo wa Rwenzururu.

Licha ya kutambua ufalme huo, watu katika eneo bado wanahisi kuwa wanabaguliw katika maswala mbalimbali.

Katika historia ya mzozo huu, Ufalme huo umekuwa ukitaka kuunda nchi yao (Jamhuri ya Yiira) kuunganisha makabila mawili, Bakonzo upande wa Uganda na Banande nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Watu wa kabila hayo mawili, yanazungumza lugha moja lakini pia wana utamaduni mmoja kutoka watu wa Ba-Yira.

Changamoto katika Ufalme wa Rwenzururu
Wachambuzi wa siasa nchini Uganda wanahisi kuwa mgogoro wa Ufalme huu unatokana na ukiukwaji wa haki za binadamu, kutengwa kimaendeleo kwa muda mrefu na suala la uogozi.

Suala la ardhi limekuwa tata sana katika eneo hilo, asilimia 60 ya ardhi katika Wilaya ya Kasese inamilikiwa na serikali na hivyo haiwanufaishi watu wa eneo hilo.

Licha ya Wilaya hiyo kuwa na utajiri wa rasilimali kama Ziwa Katwe, George na Edward. Madini mbalimbali na viwanda kama kile cha Hima, watu wengi katika Wilaya ya Kasese wanaendelea kuishi kwa umasikini na hawana ajira hasa vijana.

Jambo lingine la kutilia maanani ni kuwa eneo la Kasese na Rwenzori lina idadi kubwa ya wapiganaji walioshiriki katika vita dhidi ya Ufalme wa Tooro miaka ya 1960 lakini pia kumsaidia Museveni wakati wa vita vya msituni na sasa hivi wanahisi kuwa hawajalipwa chochote wala kukumbukwa kwa namna yoyote ile.

Suluhu
Ni lazima serikali ya Kampala izungumze na Mfalme Mumbere ili kumaliza mzozo huu ambao wengi wanaona ni wa kisiasa na unahitaji suluhu ya kisiasa.

Mazungumzo yanastahili kulenga kutatua changamoto za kiuchumi lakini pia kuangalia namna ya kushughulikia mateso ya kihistoria ambayo watu wa eneo hilo wamekuwa wakipitia.

Mfalme Mumbere lazima ashirikishwe kikamilifu katika mazungumzo hayo kwa sababu watu wengi wanamwamini mno.

Aidha, Ufalme wa Rwenzururu, hauna budi bali kutambua kuwa vita havileti bali kuja katika meza ya mazungumzo.

Wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2016, eneo hilo lilimpigia kura Kizza Besigye aliyekuwa mgombea wa upinzani na amenukuliwa akisema, mzozo huu katika Wilaya ya Kasese ni wa kisiasa na unahitaji suluhu ya kisiasa wala sio kutumia nguvu kama ilivyokuwa mwishoni mwa wiki iliyopita na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 60.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.