Pata taarifa kuu
TANZANI-DRC-KENYA

Madereva wa Tanzania na Kenya waachiliwa na waasi nchini DRC

Madereva wa Malori kutoka nchini Tanzania na Kenya waliokuwa wametekwa na waasi wa Mai-Mai katika Jimbo la Kivu Kusini siku ya Jumatano wiki hii, wameokolewa na wanajeshi wa serikali FARDC.

Malori yaliyoteketezwa moto na waasi Mashariki mwa DRC
Malori yaliyoteketezwa moto na waasi Mashariki mwa DRC dailynews.co.tz
Matangazo ya kibiashara

Waziri wa Mambo ya ndani  wa DRC Zakwani Salehe amethibitisha kuokolewa kwa madereva hao, wanane  kutoka Tanzania na wanne kutoka nchini  Kenya.

Aidha, amesema kuwa hakuna  kikombozi kilicholipwa kuwaachilia huru madereva hao.

Siku ya Alhamisi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya nje ya Tanzania Mindi Kasiga alisema kuwa  waasi hao wanataka kikombozi cha Dola za Marekani, 4,000 kutoka kwa kila dereva ili kuwaachilia huru madereva hao.

Waziri wa Mambo ya nje wa Tanzania Augustine Mahiga, ameithibitishia RFI Kiswahili kuwa madereva hao wameachiliwa huru na waasi hao bila masharti.

"Tunawashukuru sana  wanajeshi wa DRC, viongozi wa kisiasa kama Gavana wa jimbo la Kivu Kusini kwa kusaidia kuwaachilia huru madereva hao,".

Aidha, amewataka wafanyibiashara kushirikiana na serikali za Tanzania na DRC ili kupewa ulinzi wanapokuwa safarini.

Hii si mara ya kwanza kwa waasi kuwateka raia wa Tanzania.

Mwaka uliopita, wahubiri wanane wa Kiislamu pia kutoka Tanzania, walitekwa na waasi na kuachiliwa huru baada ya kufanyika kwa mazungumzo kati ya serikali ya Tanzania, DRC na waasi hao.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.