Pata taarifa kuu
SUDANI KUSINI-MACHAR

Riek Machar akimbilia jijini Kinshasa, DRC

Makamu wa rais wa zamani wa Sudan Kusini ambaye pia alikuwa kiongozi wa waasi Riek Machar, amekimbilia nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Riek Machar alipowasili mwezi Aprili tarehe 26 mwaka huu .
Riek Machar alipowasili mwezi Aprili tarehe 26 mwaka huu . REUTERS/Jok Solomun
Matangazo ya kibiashara

Duru zakuamini zinasema kuwa kikosi cha askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo kilimsaidia yeye, mke wake pamoja na watu wengine kutoka kwenye mpaka unaogawa nchi ya DRC na Sudan Kusini.

Umoja wa Mataifa umethibitisha taarif ahiyo na kubaini kwamba Makamu wa Rais wa zamani wa Sudan Kusini Riek Machar ambaye alikuwa haonekana hadharani yuko nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Mshirika wa karibu wa Machar amethibitisha kuwa kiongozi wao amewasili jijini Kinshasa na anataka kwenda nchini Ethiopia haraka iwezekanavyo.

 Machar alikimbilia mafichoni kutoka mji mkuu  Juba baada ya kuzuka kwa mapigano kati ya wanajeshi wake na wale wa rais Salva Kiir mwezi uliopita karibu na Ikulu ya rais.

Baada ya Machar  kuondoka jijini Juba na kukimbilia katika eneo lisilofahamika, rais Kiir alimteua Taban Deng Gai aliyeongoza ujumbe wa upinzani kufanikisha mazungumzo ya amani kati ya waasi na serikali  kuchukua nafasi yake, uteuzi ambao Machar alipinga na kusisitiza kuwa anaendelea kuwa Makamu wa kwanza wa rais.

Gai amekuwa ziarani nchini Kenya wiki hii na akizungumza na wanahabari siku ya Jumanne  jijini Nairobi, alimtaka Machar kuachana na siasa ili serikali itekeleze ipasavyo mkataba wa amani.

Wiki iliyopita Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio la kutuma kikosi cha wanajeshi 4000 cha kulinda amani kutoka mataifa ya Kenya, Rwanda na Ethiopia kwenda kulinda amani jijini Juba na kuhakikisha kuwa maeneo ya Umoja wa Mataifa hayavamiwi.

Kiir na Machar wameendelea kulaumiana kuhusu mzozo mpya uliotokea katika nchi yao baada ya kuanza kufanya kazi pamoja mwezi Aprili mwaka huu.

Mapigano nchini Sudan Kusini yaliyoanza rasmi mwezi Desemba mwaka 2013 jijini Juba, yamesababisha vifo vya maelfu ya watu na wengine zaidi ya Milioni 2.5 kukimbia makwao.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.