Pata taarifa kuu
SUDAN KUSINI

Marekani yataka kupelekwa haraka kwa kikosi maalumu mjini Juba

Marekani imeliomba baraza la usalama la umoja wa Mataifa kuidhinisha kutumwa kwa kikosi maalumu cha wanajeshi elfu 4 kutoka nchi za ukanda kwenda Sudan Kusini pamoja na kuiwekea nchi hiyo makataa ya kununua silaha ikiwa Serikali itakataa kupelekwa kwa wanajeshi hao. 

Askari wa umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS, wakipiga doria kwenye kambi yao, Julai 20, 2016.
Askari wa umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS, wakipiga doria kwenye kambi yao, Julai 20, 2016. REUTERS/Stringer
Matangazo ya kibiashara

Pendekezo la awali lililowasilishwa kwenye baraza la usalama, linataka kupelekwa kwa wanajeshi watakaokuwa na jukumu la kuwalinda raia na kupewa mamlaka ya kutumia nguvu inapohitajika ili kutoa usalama kwenye jiji la Juba.

Kikosi hicho pia kitakuwa na jukumu la kuzima mashambulizi yoyote ambayo yataelekezwa kwa wafanyakazi na wanajeshi wa umoja wa Mataifa.

Chini ya pendekezo hili, baraza la usalama litapiga kura kuiwekea vikwazo vya silaha Serikali ya Sudan Kusini ikiwa katibu mkuu Ban Ki Moon atatoa taarifa kuwa nchi hiyo imeweka vikwazo kupelekwa kwa wanajeshi hao.

Katibu mkuu Ban Ki Moon anatarajiwa kuwasilisha ripoti kwenye baraza la usalama ndani ya siku 14 zijazo ili azimio hili lipitishwe.

Kikosi cha ukanda kitapelekwa nchini humo chini ya uangalizi wa vikosi vya umoja wa Mataifa UNMISS, ambavyo vimekosolewa vikali kwa kushindwa kuwalinda maelfu ya raia ambao wanahifadhiwa kwenye kambi ya umoja huo.

Kikosi hiki kipya kitakuwa na jukumu la kulinda uwanja wa ndege wa Juba, kuhakikisha kunakuwa na uhuru wa watu kutembea, kuingia na kutoka mjini Juba pamoja na kujibu mashambulizi dhidi ya maofisa na makazi ya umoja wa Mataifa.

Kwa mujibu wa pendekezo hili, linazitaka nchini za ukanda kuharakisha kupelekwa kwa wanajeshi hao maalumu haraka iwezekanavyo ili kuianza kazi.

Kura ya kupitisha azimio hili inatarajiwa kufanyika wiki hii.

Mji wa Juba ulikumbwa na mapigano makali mwanzoni mwa mwezi Julai kati ya vikosi vya Serikali na vile vya waasi wa Riek Machar aliyekuwa makamu wa kwanza wa rais.

Watu zaidi ya 300 wamekufa kutokana na mapigano hayo ambapo walinda amani wawili wa China waliuawa baada ya kambi yao kushambuliwa, ambapo maelfu ya raia wanapatiwa hifadhi.

Katibu Mkuu Ban Ki Moon ametaka kuwekwa vikwazo vya silaha kwa nchi ya Sudan Kusini pamoja na kuzuia mali za viongozi wanaodaiwa kuhusika kwenye machafuko ya hivi karibuni.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.