Pata taarifa kuu
KRISMASI-WAKIRISTO-AFRIKA-DUNIA

Ujumbe wa amani watawala sherehe za Krismasi duniani

Wakristo kote duniani wanasherehekea sikukuu ya Krismasi, kuadhimisha kuzaliwa kwa mwokozi wao Yesu Kristo.

Sikukuu ya Krismasi 2019
Sikukuu ya Krismasi 2019 Church of England
Matangazo ya kibiashara

Wengi wamefurika Makanisani kuhudhuria ibada maalum huku wengine wakiamua kwenda katika maeneo ya burudani kusherehekea siku hii muhimu katika kalenda ya dini ya Kikristo.

Leo ni siku ya mapumziko katika mataifa mengi duniani, na baadhi ya watu wanatumia siku hii kutembeleana, kula pamoja na wengine kwenda kuwatembelea watu wanaoishi katika mazingira magumu na kuwapa zawadi.

Makanisani, viongozi wa madhehebu mbalimbali wametumia siku hii kutuma ujumbe wa amani hasa katika mataifa ambayo yameendelea kushuhudia ukosefu wa amani.

02:05

Ripoti ya Krismasi kutoka Tanzania

Ujumbe wa amani na utulivu umetawala nchini Jamhuri wa Kidemokrasia ya Congo, wito ukiwa kwa serikali ya rais Felix Thisekedi kuhakikisha kuwa mauaji dhidi ya raia yanayotekelezwa na makundi ya waasi hasa Wilayani Beni, yanakoma.

Katika ujumbe wa pamoja, Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis na mwenzake Justin Welby, Askofu Mkuu wa Cantebury wa Kanisa Anglikana nchini Uingereza, wamehimiza amani nchini Sudan Kusini na kuwataka viongozi nchini hiyo kutekeleza ahadi ya kuunda serikali ya pamoja, mapema mwaka 2020.

“Msimu huu wa Krismasi na mwaka mpya unapoanza, tunawatakia heri na fanaka wananchi wote wa Sudan Kusini, tukiwaombea amani na mafanikio,” Viongozi hao wamesema.

Canon Jerome Napella Kasisi wa  Kanisa Anglikana Tanzania Mtakatifu Nikolao Ilala jijini Dar es salaam, wakati wa ibada ya Krismasi Desemba 25 2019
Canon Jerome Napella Kasisi wa Kanisa Anglikana Tanzania Mtakatifu Nikolao Ilala jijini Dar es salaam, wakati wa ibada ya Krismasi Desemba 25 2019 Fredrick Nwaka

Nchini Tanzania, akisoma ujumbe maalum wa Krismasi kutoka kwa Askofu wa Kanisa Anglikana Dayosisi ya Dar es salaam, Jackson Sosthenes, Kasisi wa Mtakatifu Nikolao Ilala, Canon Jerome Napella, ametoa wito kwa Wakiristo wa Kanisa hilo kuendelea kudumisha amani katika nchi yao na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kisiasa mwaka 2020.

“Mwaka 2020 ni mwaka wa Uchaguzi, wito wangu kama Askofu na baba yenu ni kuwa, mjitokeze kwa wingi kujiandikisha, na kugombea nafasi mbalimbali ili kuwatumikia Watanzania,” alisema Askofu Sosthenes katika ujumbe wake.

Nchini Kenya, rais Uhuru Kenyatta akiwa mjini Mombasa, amewashukuru viongozi wa dini ya Kikristo kwa juhudi zao na kuhimiza umoja wa kitaifa na kupaza sauti katika vita dhidi ya ufisadi, na wakati uo huo kutoa wito wa amani na mshikamano katika taifa hilo lenye uchumi mkubwa katika eneo la Afrika Mashariki.

Stanley Ntagali Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana nchini Uganda anayemaliza muda wake, Desemba 25 2019
Stanley Ntagali Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana nchini Uganda anayemaliza muda wake, Desemba 25 2019 NBS Uganda

Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana nchini Uganda anayemaliza muda wake Stanley Ntagali, katika ujumbe wake, amelaani tabia ya watu nchini humo kuendelea kuuana kwa sababu ya mashamba.

“Watu wanauana kwa sababu ya mashamba na majirani hawali pamoja kwa sababu, watu wamekuwa wachoyo,” amesema.

“Nawaomba watu katika nchi hii, wawachague viongozi sio kwa sababu ya fedha wanazopewa ila tuwapate watu wanaoweza kufanya kazi, walio na uwezo,” aliongeza.

Naye kiongozi wa Kanisa Katoliki nchini humo, Askofu Cyprian Kizito Lwanga, amewaambia raia wa nchi hiyo kusherehekea siku hii kwa furaha.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.