Pata taarifa kuu
DRC-M23-UN

Jeshi la DRC lasema limeendelea kuthibiti ngome za waasi wa M 23

Jeshi la serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo linasema limeendelea kuchukua maeneo zaidi yaliyokuwa yanathibitiwa na waasi wa M 23 Mashariki mwa nchi hiyo ukiwemo mji wa Rutshuru na Kiwanja na sasa jeshi linathibiti ngome ya waasi hao ya Rumangabo.

Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa Jeshi la serikali Mashariki mwa nchi hiyo Kanali Olivier Hamuli ameliambia shirika la Habari la Ufaransa AFP kuwa mapigano ya siku ya Jumatatu hayakuchukua muda mrefu na tayari waasi hao wamedhoofika.

Aidha, Hamuli ameongeza kuwa wapiganaji 20 wa M 23 wamejisalimisha kwa majeshi ya FARDC mjini Kiwanja huku Ofisa wa jeshi la Umoja wa Mataifa la kulinda amani MONUSCO akisema zaidi ya waasi 70 wamejisalimisha.

Nalo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linakutana siku ya Jumatatu kuzungumzia mapigano mapya yanayoendelea Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kati ya waasi wa M 23 na majeshi ya serikali yakisaidiwa na yale ya Umoja wa Mataifa.

Kuendelea kwa mapigano hayo kumeisukuma Ufaransa kuitisha kikao hicho cha dharura huku Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon akishtumu mapambano yanayoendelea.

Mapambano hayo yalianza wiki iliyopita baada ya mazungumzo ya amani kati ya waasi hao na serikali ya DRC kukwama jijini Kampala Uganda, na  yamesababisha maelfu ya waakazi wa Mashariki kukimbia makwao na kusababisha kuuawa kwa mwanajeshi mmoja wa Umoja wa Mataifa kutoka nchini Tanzania.

Kiongozi wa jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa MONUSCO Martin Kobler amesema kuwa mwanajeshi huyo wa Tanzania aliuawa wakati akiwalinda raia katika mji wa Kiwanja na anakuwa mwanajeshi wa tatu kutoka nchini Tanzania kuuawa katika mapambano hayo.

Awali, Msemaji wa jeshi la Serikali Mashariki mwa nchi hiyo Kanali Olivier Hamuli, aliiambia RFI Kiswahili kuwa vikosi vya serikali vimefanikiwa pakubwa kuwarudisha waasi wa M 23 na sasa wanathibiti miji ya Rutshuru na Kiwanja.

Hata hivyo, waasi wa M 23 kwa upande wao wanasema kuwa walijiondoa katika eneo la Kiwanja kwa lengo la kuwalinda raia na hawakusukumwa nyuma na wanajeshi wa serikali.

Msemaji wa waasi hao Amani Kabasha analishtumu jeshi la serikali kuwavamia katika ngome zao na kusababisha mapigano hayo madai yanayokanusha na majeshi ya serikali yanayosema kuwa waasi ndio walianza kuwavamia.

Wiki iliyopita,  Rwanda nayo iliishutumu jeshi la DRC kwa kutupa makombora katika ardhi yake na kutishia kulipiza kisasi ikiwa hali itaendelea kuwa hivyo.

Umoja wa Mataifa unaushtumu Rwanda kuwaunga mkono waasi wa M 23 madai ambayo serikali ya Kigali imeendelea kukanusha.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.