Pata taarifa kuu
MAREKANI

Mazungumzo ya Rais Obama na Viongozi wa Republican yagonga mwamba juu ya kusaka mbinu za kupitisha bajeti ya serikali

Serikali ya Marekani huenda ikawa kwenye wakati mgumu kwa muda zaidi kutokana na mazungumzo yaliyofanyika baina ya Rais Barack Obama na Viongozi wa juu wa Chama Cha Republican kushindwa kufikia muafaka huku kila upande ukionekana kunyosha kidole cha lawama kwa mwingine.

Rais wa Marekani Barack Obama anaendelea na juhudi za kuwashawishi Wabunge wapitishe bajeti mpya ya Serikali
Rais wa Marekani Barack Obama anaendelea na juhudi za kuwashawishi Wabunge wapitishe bajeti mpya ya Serikali REUTERS/Jason Reed
Matangazo ya kibiashara

Rais Obama alifanya mazungumzo ya faragha katika Ikulu ya White House na Viongozi wa Chama Cha Republican lengo lake likiwa ni kuwashawishi wapitishe bajeti mpya ya serikali ambayo ingesaidia kufunguliwa kwa shughuli nyingi zilizolazinika kufungwa kutokana na Serikali kukosa pesa.

Viongozi wa Juu wa Chama Cha Republican wameendelea kushikilia msimamo wao wa kutokuwa tayari kupitisha bajeti mpya ya serikali hadi pale ambapo sheria mpya ya matibabu iliyopitishwa na Rais Obama itakapofanyiwa mabadiliko kwani imekuwa mzigo kwa taifa.

Rais Obama ameendelea kukaza kamba na kusema hayupo tayari kufanya mabadiliko kwenye sheria hiyo mpya ya matibabu kwani imekuwa mkombozi kwa wananchi wengi wa Marekani waliokuwa hawana uwezo wa kupata huduma hiyo muhimu.

Mazungumzo kati ya Rais Obama na Spika wa Bunge John Boehner na Kiongozi wa wachache Bungeni Mitch McConnell yalidumu kwa zaidi ya saa moja lakini hakukuwa na muafaka uliofikiwa baina ya pande hizo mbili kitukinachoongeza hofu ya kutetereka kwa uchumi wa Marekani.

Spika Boehner baada ya kumalizika mazungumzo hayo akajitokeza na kuzungumza na wanahabari na kuwaeleza Rais Obama anahitaji muda zaidi ili kuhakikisha anafanya nao mazungumzo ambayo yanaweza yakaleta suluhu ya kile kinachoendelea.

Msemaji wa Ikulu ya White House Jay Carney punde baada ya kushindwa kufikiwa muafaka kwa mazungumzo hayo kati ya Rais Obama na Viongozi wa Chama Cha Republican akatoa taarifa na kusema kuna matumaini muafaka utafikiwa pale ambapo wabunge wataonesha kujitambua.

Serikali ya Marekani imelazimika kufunga shughuli zake zote ukiondoa zile za vyombo vya usalama na matibabu kutokana na kukosa fedha za kuendesha shughuli hizo kutokana na bajeti mpya kukwama.

Wafanyakazi wa umma wanaofikia Laki Saba wameshindwa kulipwa mishahara yao na wengi wapo hataraini kupoteza ajira zao iwapo bajeti hiyo mpya itaendelea kukwama kupitishwa na Bunge.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.