Pata taarifa kuu
MAREKANI-KOREA KASKAZINI-USALAMA

Trump : Mkutano wetu umekua wa mafanikio makubwa

Rais wa Marekani Donald Trump amesema mkutano wake wa kihistoria kati yake na kiongozi wa Korea Kaskazini, umekuwa wa mafanikio makubwa nchini Singapore.

Rais wa Marekani Donald Trump akiongea katika mkutano na waandishi wa habari baada ya kukutana na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un katika Hoteli ya Capella katika kisiwa cha Sentosa huko Singapore Juni 12, 2018.
Rais wa Marekani Donald Trump akiongea katika mkutano na waandishi wa habari baada ya kukutana na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un katika Hoteli ya Capella katika kisiwa cha Sentosa huko Singapore Juni 12, 2018. Reuters/路透社
Matangazo ya kibiashara

Mkutano kati ya rais Trump na Kim Jong UN umeelezwa kuwa wa kihistoria kwa sababu, imekuwa mara ya kwanza kwa viongozi wa mataifa haya mawili, ambayo yamekuwa yakitishana, kukutana na kupeana mikono kama ishara ya kufungua ukurasa wa ushirikiano mpya kwa ajili ya amani.

Baada ya mkutano wa saa kadhaa, rais Trump na Kim Jong Un, walitia saini mkataba wa maelewano, kikubwa kikiwa ni kukubali kwa Korea Kaskazini kuachana kabisa na mradi wake wa kutengeneza silaha za nyuklia.

Kitu kingine kilichokubaliwa, ni kwa Marekani kusitisha mazoezi ya kijeshi na Korea Kusini, mazoezi ambayo kwa muda mrefu Korea Kusini imekuwa ikisema ni uchokozi.

Kim Jong Un amesema, ameepuka vikwazo vingi kukutana na rais wa Marekani huku Trump akisema, anaamini kuwa Korea Kaskazini itaanza kutekeleza mpango wa kuachana na mradi wake wa nyuklia mara moja, huku akiahidi kuwa Marekani itahakikisha kuwa Korea Kaskazini inakuwa salama.

Hata hivyo, wachambuzi wa mambo wanaoana kuwa makubaliano hayo hayana uzito kwa sababu hayajaelezea ni vipi Korea Kaskazini itaacha kutekeleza mradi wake wa nyuklia, lakini rais Trump amefafanua kuwa Marekani itatuma wawakilishi wake kuthibitisha hilo.

Rais wa Korea Kusini Moon Jae-in amesifu makubaliano hayo na kusema kukutana kwa viongozi hao wawili, kutaandika historia mpya ya amani kati ya nchi yake na Korea Kaskazini.

Viongozi wa China na Japan nao pia wamesifu mkutano huu na kueleza kuwa wa kihistoria.

Kinachosubiriwa sasa ni kuona iwapo makubaliano kati ya rais Trump na Kim Jong Un yatatekelezwa, na yatakuwa na matokeo gani kwa amani ya dunia.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.