Kim Jong Un ataka kuandika historia ya kumaliza mvutano na Korea Kusini
Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un amekutana na ujumbe kutoka Korea Kusini na kusema lengo lake ni kufanikisha mazungumzo kati ya nchi hizo mbili.
Imechapishwa:
Kim Jong-un amesema anataka kuacha historia ya kuunganisha Korea Kaskazini na Korea Kusini na kumaliza wasiwasi wa kiusalama dhidi ya jirani yake kutokana na mradi wake wa nyuklia.
Kingozi huyo amekutana na ujumbe wa Korea Kusini na kula nao chakula cha jioni, kikiwa ni kikao cha kwanza kati ya ujumbe wa Seoul na kiongozi huyo wa Pyongyang tangu alipoingia madarakani mwaka 2011.
Uhusiano kati ya nchi hizi mbili umeonekana umeanza kuimarika tangu michezo ya Olimpiki ya msimu wa baridi iliyofanyika nchini Korea Kusini.
Kabla ya kuanza kwa michezo hiyo, Korea Kusini ilikubali kuja kwa wachezaji wa Korea Kaskazini katika michezo hiyo na hata kuunda timu moja ya mchezo wa magongo.
Mkutano huu umetoa matumaini ya kuendelea kufanyika kwa mazungumzo zaidi katika siku zijazo ili kuondoa wasiwasi wa kiusalama kati ya Pyongyang na Seoul.