Pata taarifa kuu
PAKISTAN-UFISADI

Waziri Mkuu wa Pakistan Nawaz Sharif ajiuzulu

Nawaz Sharif amejiuzulu kama Waziri Mkuu wa Pakistan baada ya uamuzi wa Mahakama ya Juu nchini humo.

Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Pakistan  Nawaz Sharif
Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Pakistan Nawaz Sharif REUTERS/Carlo Allegri
Matangazo ya kibiashara

Uamuzi wa Mahakama umekuja baada ya kubainika kuwa Sharif pamoja na familia walikuwa ni miongoni mwa watu walioficha fedha za umma nje ya nchi kwa manufaa yao binafsi.

Ripoti maarufu inayofahamika kama Panama Papers ilieleza kuwa, Sharif alikuwa ni miongoni mwa watu wengine mashuhuri duniani waliohusika katika sakata hilo.

Panama ni taifa dogo katika bara la Amerika ya Kati.

Hata kabla ya kutolewa kwa uamuzi huu, Sharif amekuwa akikanusha kuhusika katika sakata hilo.

Majaji watano jijini Islamabad wamesema baada ya kusikiliza kwa makini na kuangalia ushahidi uliokuwa mbele yao, wamebaini kuwa ni kweli Sharif alihusika na hivyo amekosa uaminifu kwa wananchi wa taifa hilo.

Maelfu ya wanajeshi na polisi wanapiga doria jijini Islamabad kwa hofu kuwa huenda machafuko yakazuka baada ya uamuzi huo wa Mahakama na kujiuzulu kwa Sharif.

Pakistan imeendelea kuwa na historia ya Mawaziri Wakuu kujiuzulu. Nawaz Sharif ambaye amekuwa Waziri Mkuu tangu mwaka 2013, amekuwa Waziri wa 18 kujiuzulu bila ya kumaliza muhula wake.

Wachambuzi wa siasa nchini Pakistan wanasema uamuzi wa Mahakama ni ishara kuwa idara hiyo imeanza kupambana na ufisadi bila ya kuangalia nafasi alio nayo mtu katika jamii.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.