Korea Kaskazini yasisitiza kuwa iko tayari kujibu mashambulizi ya Marekani
Korea Kaskazini inasema iko tayari kujibu mashambulizi yoyote kutoka kwa Marekani.
Imechapishwa:
Choe Ryong-Hae afisa wa juu wa serikali ya Pyongyang amesema, jeshi la nchi yake lipo tayari kuikabili Washington DC kwa kutumia silaha zake za Nyuklia.
Kauli hii imekuja wakati nchi hiyo ikiadhimisha miaka 105 ya kumbukumbuka kiongozi wa kwanza wa taifa hilo Kim Il-Sung siku ya Jumamosi.
Kiongozi wa sasa Kim Jong-Un amekagua gwaride la maefu ya wanajeshi wa taifa hilo jijini Pyongyang, katika maadhimisho hayo huku wanajeshi wakionesha silaha za kivita.
Rais wa Marekani Donald Trump amekuwa akionya kuishambulia Korea Kaskazini kijeshi kwa sababu ya silaha zake za Nyuklia.
Tayari jeshi la Marekani likiwa na manuari za kivita limepiga kambi Baharini karibu na mpaka na Korea Kaskazini.
China ambaye ni mshirika wa karibu wa Korea Kaskazini imesema inahofia sana hali ya wasiwasi inayoshuhudiwa na kuongeza kuwa ni kweli vita vinaweza kutokea.
Hata hivyo, Beijing ambayo inataka mzozo kati ya mataifa hayo mawili kutatuliwa kwa amani, inasema hakuna atakayekuwa mshindi ikiwa vita vitakavyotokea.