Pata taarifa kuu
JAPAN-MAREKANI-KOREA KASKAZINI

Trump, Shinzo Abe watofautiana kuhusu suala la Korea Kaskazini

Waziri mkuu wa Japan, Shinzo Abe ameonesha wazi kutofautiana na rais wa Marekani Donald Trump kuhusu njia muafaka ya kushughulikia suala la mpango wa nyuklia la Korea Kaskazini.

Rais wa Marekani, Donald Trump akiwa na mwenzake wa Japan Shinzo Abe wakati wa ziara yake nchini JapanTokyo, Japan May 26, 2019.
Rais wa Marekani, Donald Trump akiwa na mwenzake wa Japan Shinzo Abe wakati wa ziara yake nchini JapanTokyo, Japan May 26, 2019. Kiyoshi Ota/Pool via Reuters
Matangazo ya kibiashara

Wakizungumza na waandishi wa habari katika mkutano wao wa pamoja, rais Trump ameendelea kusisitiza msimamo wake wa kuheshimu urafiki alioanza kuujenga na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un.

Rais Trump amesema licha ya mazungumzo ya hivi karibuni kugonga mwamba, bado anaamini kuwa Kim Jong Un anayo nafasi ya kufanya jambo sahihi kwa kuachana na mpango wake wa nyuklia.

Kwa upande wake waziri mkuu Shinzo Abe amesema namna rais Trump anavyoshughulikia suala la Korea kaskazini ni hatari kwa usalama wa kikanda na kwamba ni lazima kiongozi huyo aoneshe kuwa yuko makini katika kuhakikisha Korea Kaskazini haimiliki silaha za maangamizi.

Waziri mkuu Abe ametolea mfano jaribio la hivi karibuni la Korea Kaskazini, ambapo amesema kitendo kilichofanywa na taifa hilo kinakiuka sheria za kimataifa na imani ambayo tayari mataifa yao yalikuwa yameonesha kwa nchi hiyo.

Haya yanajiri wakati huu Serikali ya Pyongyang ikimkashifu mshauri wa masuala ya usalama wa taifa wa Marekani John Bolton, ambaye imemuita kama “mpenda vita.”

Mwishoni mwa juma Botlon alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa kutendo cha Korea Kaskazini cha juma moja lililopita cha kufanya jaribio la silaha zake kilikiuka sheria za kimataifa.

Korea Kaskazini inamuona Bolton kama mtu ambaye amekuwa akikwamisha mazungumzo yao na rais Trump sambamba na waziri wa mambo ya nje Mike Pompeo ambao wamekuwa na msimamo mkali kuhusu Korea Kaskazini.

Hata hivyo licha ya kuuokosoa utawala wa Pyongyang, Serikali ya Washington imesema bado iko tayari kuwa na mazungumzo na Korea Kaskazini licha ya kile ilichosema ni tabia mbaya ya utawala wa Kim Jong Un.

Wachambuzi wa mambo wanaona kuwa mpango wa rais Trump kuishawishi Korea Kaskazini kuachana na urutubishaji wa Urani unagonga mwamba kwa kile wanasema ni ushawishi ambao mataifa ya Urusi na China inao kwa utawala wa Pyongyang.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.