"Moja ya hatari za mtandao ni kwamba watu wanaweza kuona hali halisi tofauti kabisa, na kupata habari zinazokinzana," Obama amesema katika mahojiano hayo ya kwanza tangu kuondoka kwake madarakani mnamo mwezi Januari.
Alielezea wasi wasi kuhusu siku za usoni ambapo ukweli utapotoshwa na watu watakuwa wakisoma na kusikiliza vitu ambavyo vitakuwa vikiridhisha maoni yao.
Bw Obama alionya kuwa vitendo kama hivyo vinachanganya uelewa wa watu katika masuala magumu na kusambaza uvumi.
"Swali ambalo mtu anapaswa kujiuliza, vipi unaweza kutumia teknolojia hii ili kuruhusu wingi wa sauti, utofauti wa maoni, huku ukiepuka kuminya jamii," Barack Obama ameongeza, bila kutaja mrithi wake Donald Trump , anaekosolewa kwataarifa zake anazorusha kwenye twitter.
Barack Obama amesema wale walio katika nyadhifa za uongozi wanastahili kuwa waangalifu wakati wanaandika katika mitandao.