Pata taarifa kuu
IRAN-MAREKANI-SAUDI ARABIA

Iran yakanusha vikali madai kuwa inatoa silaha kwa waasi wa Yemen

Nchi ya Iran imekanusha vikali madai kuwa imekuwa ikiwasaidia kwa silaha waasi wa Yemen, silaha ambazo wamezitumia kushambulia nchi ya Saudi Arabia, madai yanayotolewa na Riyadh na Serikali wa Washington.

Rais wa Iran Hassan Rouhani
Rais wa Iran Hassan Rouhani ©REUTERS/Stephanie Keith
Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Iran Bahram Ghasemi ameliambia shirika la habari la nchi hiyo kuwa “hatuna uhusiano wowote wa silaha na nchi ya Yemen” matamshi aliyoyatoa baada ya nchi ya Saudi Arabia kudai kuwa hapo jana ilifanikiwa kudungua roketi iliyorushwa nchini mwake.

Msemaji huyo ameongeza kuwa tuhuma dhidi ya nchi yao kuwa inawasaidia waasi wa Yemen kwa silaha ni uongo mkuu.

Iran inasema nchi ya Yemen iko kwenye orodha ya umoja wa Mataifa ya nchi ambazo zimezuiwa kuuziwa wala kununua silaha na hivyo hakuna uwezekano wowote wa waasi hao kupata silaha.

Shambulio la roketi lililorushwa hapo jana na waasi wa Yemen limekuja ikiwa ni mwezi mmoja tu umepita toka Saudi Arabia ifanikiwa kuangusha roketi nyingine iliyokuwa imerushwa kulenga uwanja wa ndege wa Riyadh.

Iran inasisitiza kuwa silaha zinazotumiwa na waasi kukabiliana na nchi washirika na Saudi Arabia ambazo zimekuwa zikiendesha mashambulizi dhidi ya waasi wa Houthi ni mabaki ya silaha za utawala uliokimbia Sanaa.

Nchi ya Saudi Arabia na washirika wake wamekuwa wakikabiliana na waasi wa Yemen tangu mwaka 2015 na mara zote wamekuwa wakiituhumu Iran kuwafadhili kwa silaha waasi hao.

Saudi Arabia inasema silaha zinazotolewa na Iran na hasa roketi ambazo zimekuwa zikitumiwa na waasi hao ni hatari kwa usalama wa ukanda.

Balozi wa Marekani kwenye umoja wa Mataifa Nikki Haley amesema kitendo kinachofanywa na Iran kuwasaidia waasi kwa silaha hakikubaliki na kwamba ishara zote zinaonesha mashambulizi yaliyotekelezwa na waasi hao zilitengenezwa nchini Iran.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.