Trump abadilisha mtazamo wake kuhusu jeshi la NATO
Rais wa Marekani Donald Trump ameonesha kubadilisha msimamo wake kuhusu jeshi la muungano wa nchi za Mataifa ya Magharibi NATO.
Imechapishwa:
Trump amesema jeshi hilo ni muhimu sana kutokana na ongezeko la visa vya ugaidi vinavyongezeka katika maeneo mbalimbali duniani na haliwezi kupuuzwa.
Kiongozi huyo wa Marekani aliyekutana na Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg katika Ikulu ya White House, amelitaka jeshi hilo kuzidisha makabiliano dhidi ya makundi ya kigaidi hasa nchini Iraq na Afganistan.
Wakati wa kampeni ya kuwa rais mwaka uliopita, Trump alinukuliwa akisema haoni umuhimu wowote wa jeshi la NATO huku akisema Marekani imeendelea kutumia fedha nyingi kulifadhili.
Stoltenberg amesema kuwa mazungumzo yake na rais Trump yalikwenda vizuri na walizungumza mengi kuhusu namna NATO inavyoweza kuisaidia kupambana na ugaidi.
Hata hivyo, Trump ameyataka mataifa yanayochangia katika jeshi hilo kusaidia kuchangia fedha kufanikisha operesheni za NATO.