Pata taarifa kuu
TANZANIA

Tanzania: 20 wapoteza maisha katika mkutano wa dini, nabii ahojiwa

Polisi nchini Tanzania wanamuhoji kiongozi mmoja wa dini mashuhuri nchini humo, Boniface Mwamposa, baada ya siku ya Jumamosi wakati wa mkutano wake wa injili watu 20 kupoteza maisha kwa kukanyagana na wengine zaidi ya 16 kujeruhiwa.

Picha ikimuonesha Nabii Boniface Mwamposa, akiwa katika kanisa lake la Arise and Shine. Picha kwa hisani ya tovuti rasmi ya kanisa lake
Picha ikimuonesha Nabii Boniface Mwamposa, akiwa katika kanisa lake la Arise and Shine. Picha kwa hisani ya tovuti rasmi ya kanisa lake www.ariseandshine.or.tz
Matangazo ya kibiashara

Tukio hilo lilitokea wakati mtumishi huyo alipowataka waumini wake kupita katika eneo ambako alikuwa amemwaga kile kinachoaminika kuwa mafuta ambayo ikiwa waumini wangekanyaga basi wangepokea uponyaji.

Hata hivyo kwa mujibuj wa vyanzo mbalimbali likiwemo jeshi la polisi mkoani Kilimanjaro ambako tukio hili lilitokea, eno ambalo mtumishi huyo alimwaga mafuta halikuwa na miundo mbinu ambayo ingeruhusu waumini wengie zaidik kupita kwa wakati mmoja.

Polisi mkoani Kilimanjaro wanasema kutokana na msongamano mkubwa wa watu waliokuwa wakitaka kukanyaga mafuta hao, baadhi walianguka na kuanza kukanyagwa na waumini wengine ambao nao walikuwa wakijaribu kufika katika eneo ambako mafuta hayo yalikuwa yamemwagwa.

Mkuu wa wilaya ya Moshi Kippi Warioba amesema huenda idadi ya vifo ikaongezeka kutokana na wengi wa waliojeruhiwa kuwa katika hali mbaya wakiendelea kupatiwa matibabu.

β€œMpaka sasa ni watu 20 wamekufa, lakini idadi hii huenda ikaongezeka kutokana na watuj wengi pia kujeruhiwa,” alisema Warioba.

Tayari polisi mkoani Kilimanjaro wamemuita mtumishi huyo kwa mahojiano baada ya yeye kuwa ameondoka kwenye eneo la tukio punde baada ya kumaliza ibada yake.

Awali polisi mkoani Kilimanjaro walisema walikuwa wanamsaka mtumishik huyo kwakuwa waliamini alikuwa ametoroka eneo la tukio kabla ya kuonekana jijini Dar es Salaam katika kanisa lake liliko eneo la Kawe akiaga waumini akisema anaitikia wito wa jeshi la polisi.

Tayari rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli, ametuma salamu za rambi rambi kwa familia ambazo zimepoteza ndugu zao katika tukio hilo na kutoa wito kwa viongozi wa dini nchini humo kuwa makini wakati wa mikutano yao ikiwa ni pamoja na wananchi kuchukua tahadhari pale wanapoona kuna viashiria vya kutokea hatari.

Nchi ya Tanzania ni miongoni mwa mataifa mengi hapa barani Afrika ambayo katika siku za hivi karibuni kumekuwa na wimbi kubwa la kujitokeza kwa viongozi wa dini wanaojipambanua kama manabii na kudai kuwa na uwezo wa kuwaponya wagonjwa kwa kutumia mafuta au maji.

Kufuatia tukio hili viongozi kadhaa wa dini nchini humo wamependekeza hata uwepo wa sheria itakayotoa miongozi kwa viongozi wa dini kufanya kazi, baadhi wakisema wengi wanaojiita manabii hawana elimu ya kutosha kuhusu Biblia.

Mmoja wa wachungaji ambaye pia ni mwanasiasa na mbunge wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Peter Msigwa, ameandika kwenye ukurasa wake wa kijamii wa Twitter β€œWakati umefika Sasa kwa Tanzania kutunga sheria Kuwa wahubiri wote wawe na kiwango cha elimu cha kutosha cha neno la Mungu. Haya maafa yaliyotokea ni mchanganyiko wa ujinga na umaskini. Yangeweza kuepukika kama mhubiri Mwamposya angekuwa na mafunzo sahihi ya Bibilia”.

Mikutano mingi ya wahubiri maarufu nchini Tanzania imekuwa ikivutia mamia ya waumini huku baadhi ikishuhudia kutokuwepo kwa utaratibu mzuri ambao unawezesha na kutoa usalama kwa watu wanaohudhuria.

Kumekuwa na mijadala ambayo inaendelea kwenye mitandao ya kijamii nchini humo, baadhi wakikejeli na wengine kukosoa namna ambavyo baadhi ya wanaojiita manaabii wamekuwa wakitumia umasikini wa wananchi kuwapotosha kwa kuwaahidi kuwa wakisali kwao watapata mafanikio ya haraka.

Kanisa la Mwamposa linalofahamika kama β€œInuka, Uangaze” ni miongoni mwa makanisa ambayo yana maelfu ya waumini ikiwemo viongozi wa Serikali.

Hili ni tukio baya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya nchi ya Tanzania kwa watu wengi zaidi kupoteza maisha katika kongamano la kidini.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.