Mwendesha Mashtaka wa ICC aonya dhidi kuongeza kwa machafuko Guinea
Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) Fatou Bensouda, ameonya wale wote wanaohusika na kuongezeka kwa machafuko nchini Guinea.
Imechapishwa:
Fatou Bensouda ameitaka serikali na upinzani kuanza tena mazungumzo baada ya maandamano mabaya kuwahi kutokea katika nchi hiyo ndogo maskini barani Afrika.
Mvutano mkubwa unaendelea kuikumba Guinea baada ya wiki kadhaa za maandamano yaliyoandaliwa na upinzaji ambao unamshtumu Rais Alpha Condé kutaka kuwania muhula wa tatu.
"Kufuatia ripoti za matukio kadhaa ya machafuko nchini Guinea katika wiki chache zilizopita, natoa wito kwa viongozi wote na wafuasi wao wajiepushe na vurugu na waanze mazungumzo ili kukomesha hali ya uhasama inayoendelea nchini humo," amesema Mwendesha mashtaka wa ICC, Fatou Bensouda.
"Yeyote anayetenda, kuamuru, kuhamasisha, kuhimiza au kuchangia kwa njia yoyote kutenda uhalifu wa wazi ... atakabiliwa na mashtaka kwenye mahkama za Guinea au ICC," Fatou Bensouda ameonya.
Kwa jumla, raia wasiopungua 16 na afisa mmoja wa polisi wameuawa katika maandamano makubwa ambayo Guinea - nchi ndogo, maskini yenye wakaazi milioni 13 - inaendelea kukabiliana nayo tangu Oktoba 14. Watu wengi wamejeruhiwa, na wengine kadhaa wamekamatwa na kuhukumiwa.
Katiba ya Guinea inaweka kikomo cha mihula miwili kwa rais madarakani.