Pata taarifa kuu
DRC-EU-UBELGIJI-USHIRIKIANO

DRC: Felix Tshisekedi ataka kuboresha uhusiano na Umoja wa Ulaya

Kwa siku ya nne ya ziara yake nchini Ubelgiji, Rais wa DRC Felix Tshisekedi Tshilombo amekutana na Rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya anayemaliza muda wake, Jean-Claude Juncker.

Felix Tshisekedi akizungumza na raia wa DRC waishio katika nchi za kigeni, Septemba 18, Brussels.
Felix Tshisekedi akizungumza na raia wa DRC waishio katika nchi za kigeni, Septemba 18, Brussels. © THIERRY ROGE / BELGA / AFP
Matangazo ya kibiashara

Uhusiano kati ya Umoja wa Ulaya na mtangulizi wake, Joseph Kabila, ulikuwa mbaya, hasa mwishoni mwa muhula wake wa pili na wa mwisho. Mwakilishi wa Umoja wa Ulaya mjini Kinshasa alifukuzwa. Tangu wakati huo hakuna msaada wowote wa moja kwa moja kwenye bajeti ya serikali kutoka Umoja wa Ulaya. Hata hivyo Joseph Kabila bado ana ushawishi katika serikali ya DRC. Hivi karibuni Rais Felix Tshisekedi alikubali kuungana na muungano wa Joseph kabila (FCC) katika kuendesha shughuli za serikali.

Lakini ikiwa Felix Tshisekedi Tshilombo anataka kutimiza ahadi zake, atahitaji msaada kutoka Umoja wa Ulaya, ambaye ni mshirika wake.

Mapema wiki hii mjini Brussels, rais wa DRC aliwaambia wajasiriamali wa Ubelgiji, ana imani kwamba Ubelgiji itamsaidia kwa njia zote kuanza tena ushirikiano na Umoja wa Ulaya.

Kabla ya kutangazwa mshindi, Felix Tshisekedi kwenye mitandao ya kijamii, alisema anachukizwa na hatua ya kumfukuza balozi wa Umoja wa Ulaya katikati ya mchakato wa uchaguzi. Aliahidi "kumrejesha akichaguliwa kuwa rais" na kufungua upya taasisi ya "Schengen House". Bado hadi leo ujumbe huu umesalia kwenye akaunti yake ya twitter.

Lakini Felix Tshisekedi haficha kwamba anahitaji msaada kutoka washirika wake ili kuleta mabadiliko aliyoahidi. Hata hivyo, kwa upande wa Umoja wa Ulaya, kuna baadhi ya mashirika yasiyo ya kidserikali bado yanakosoa mchakato wa uchaguzi, nchi wanachama zimeendelea kugawanyika: kwa upande mmoja kuna nchi ambazo zinataka kumuunga mkono rais mpya wa DRC, kwa upande mwingine kuna nchi ambazo zinasema kuwa zina wasiwasi kuona muungano wa Joseph Kabila unanufaika kupitia msaada huo.

Katika mahojiano na gazeti la Ubelgiji, Le Soir, Felix Tshisekedi ametoa wito kwa Umoja wa Ulaya kulegeza vikwazo dhidi ya washirika wa karibu wa Joseph Kabila. Hili ni suala jingine linalozua mjadala kati ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya.

Soma zaidi: Umoja wa Ulaya walaani hatua ya DRC kumfukuza balozi wake

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.