Pata taarifa kuu
ZIMBABWE-MUGABE-SIASA

Mvutano kuhusu mahala atakapozikwa Mugabe waendelea Zimbabwe

Siku moja baada ya familia ya rais wa zamani wa Zimbabwe Robert Gabriel Mugabe kutangaza kwamba kiongozi wao atazikwa mwanzoni mwa wiki ijayo kijiji kwake Kutama, serikali imesema kiongozi huyo wa zamani atazikwa kwenye makaburi ya kitaifa ya mashujaa jijini Harare.

Raia wa Zimbabwe wanatoa heshima zao za mwisho kwa kiongozi huyo wa zamani wa Zimbabwe.
Raia wa Zimbabwe wanatoa heshima zao za mwisho kwa kiongozi huyo wa zamani wa Zimbabwe. REUTERS/Philimon Bulawayo
Matangazo ya kibiashara

Mugabe alifariki akiwa na umri wa miaka 95 na mwili wake uliwasili Jumatano wiki hii nchini Zimbabwe kutokea Singapore.

Familia ya rais huyo wa zamani Robert Mugabe imesema atazikwa mwanzoni mwa wiki ijayo nyumbani kwake Kutama, kaskazini-magharibi mwa mji wa Harare na sio kwenye makaburi ya kitaifa ya mashujaa wa ukombozi.

Kwa wakati huu raia wa Zimbabwe wanatoa heshima zao za mwisho kwa kiongozi huyo wa zamani wa Zimbabwe. Rais Emmerson Mnangagwa na maafisa wengine wa serikali walifika nyumbani kwa rais huyo jana Alhamisi.

Mwili wa Mugabwe unaendelea kuonyeshwa kwenye maeneo mbalimbali ya kihistoria tangu Ahamidi wiki hii.

Mugabe aliitawala Zimbabwe kuanzia uhuru mwaka 1980 hadi alipopunduliwa mwaka 2017.

Wakati wa utawala wake wa miaka 37, Zimbabwe iliporomoka kutoka taifa lililostawi hadi mgogoro wa kiuchumi.

Viongozi 10 kutoka Afrika wanatarajiwa kuhudhuria shughuli ya maziko ya Robert Gabriel Mugabe. Taarifa hii imetolewa na msemaji wa serikali Alhamisi wiki hii.

Mwili wa kiongozi huyo wa vita vya msituni alieongoza mapambano ya kukomesha utawala wa wazungu wachache katika nchi hiyo iliyokuwa inaitwa Rhodesia, ulirudishwa Zimbabwe Jumatano ukitokea Singapore alikofariki.

Miongoni mwa viongozi wa Afrika waliothibitisha kushiriki katika shughuli hiyo ni pamoja na rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa,Uhuru Kenyatta wa Kenya,na Filipe Nyusi wa Msumbiji. Marais wastaafu watakaoshiriki ni pamoja na Jacob Zuma wa Afrika Kusini,Kenneth Kaunda wa Zambia na Sam Nujoma wa Namibia.

Serikali ya Zimbabwe imesema Mugabe atazikwa Jumapili katika makaburi ya mashujaa wa kitaifa mjini Harare lakini familia ya kiongozi huyo wa zamani inataka kumzika karibu na kaburi la mamayake kama alivyotaka mwenyewe,katika kijiji cha Kutama,kiasi kilomita 85 kutoka mji mkuu Harare. Msemaji wa familia ya Mugabe pia amesema maziko yatafanyika wiki ijayo jumatatu au Jumanne.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.