Chama cha front populaire pour la rennaissence de la centreafrique (FPRC) kimesema katika taarifa yake kwamba viongozi wa serikali wameshindwa kutekeleza makubaliano kwa kuunda serikali mpya, badala yake wamerejesha serikali iliokuwepo.
Mapema Jumapili serikali mpya iliundwa kulingana na makubaliano ya amani ambayo yaliagiza uundwaji wa serikali ya Umoja wa kitaifa, lakini hata hivyo hakuna kilichobadilika washiriki ni walewale.
Kwa mujibu wa Noureddine Adam mwenyekiti wa chama cha FPRC, rais wa Jamauhuri ya Afrika ya Kati amezika matarajio ya wananchi wa taifa hilo ambao walitarajia kuona mabadiliko kwenye nyadhifa mbalimbali.
Kundi hilo limetangaza kuwa halitashiriki kwenye serikali hiyo, licha ya kutoweka wazi kwamba limejitoa kwenye kamati inayofuatilia utekelezwaji wa makubaliano ya amani ya huko Kharthoum.
Makundi ya waasi ambayo yaliomba kupewa nafasi ya waziri mkuu, jambo ambalo lilitekelezwa, lakini kwenye wizara nyingine muhimu za serikali iliotengazwa kupitia radio ya taifa yamejikuta yametengwa.