Pata taarifa kuu
DRC-SIASA-UCHAGUZI

Raia wa DRC wapiga kura katika Uchaguzi wa kihistoria

Mamilioni ya wapiga kura nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wanapiga kura katika uchaguzi wa kihistoria, unaofanyika siku ya Jumapili.

Kituo cha kupigia kura nchini DRC
Kituo cha kupigia kura nchini DRC http://www.rfi.fr/
Matangazo ya kibiashara

Tume ya Uchaguzi CENI, imesema wapiga kura Milioni 40 wana nafasi ya kuwachagua viongozi wao akiwemo rais na wabunge katika uchaguzi ambao ulistahili kufanyika mwaka 2016.

Hata hivyo, wapiga kura Milioni 1.3 hawatapiga kura katika maeneo ya Beni, Butembo na Yumbi kwa hofu ya ugonjwa wa Ebola na hali ya usalama.

Jijini Kinshasa, wapiga kura wameamkia mvua kubwa, iliyosababisha barabara kujaa maji na kusababisha wapiga kura kushindwa kufika katika vituoni kwa wakati.

Mpiga kura jijini Kinshasa
Mpiga kura jijini Kinshasa © REUTERS / Baz Ratner

Maeneo ya mashariki mjini Goma na Bukavu, waandishi wa RFI Kiswahili wameripoti kuwa, zoezi limeanza vema lakini mashine za kupigia kura zinafanya kazi taratibu.

Siku ya Jumamosi, wagombea wa upinzani walikataa kutia saini mkataba wa kuhimiza amani, kipindi hiki cha Uchaguzi, licha ya wito kutoka kwa muungano wa nchi za Kusini mwa bara la Afrika SADC.

Wagombea 21 wanawania urais kumrithi rais Joseph Kabila ambaye anaondoka madarakani baada ya miaka 17.

Wagombea wakuu wa urais ncjini DRC, Martin Fayulu (Kushoto), Emmanuel Ramazani Shadary (Katikati) na Felix Tshisekedi (Kulia)
Wagombea wakuu wa urais ncjini DRC, Martin Fayulu (Kushoto), Emmanuel Ramazani Shadary (Katikati) na Felix Tshisekedi (Kulia) AFP

Hata hivyo, ushindani ni kati ya wagombea watatu ambao ni pamoja na Emmanuel Ramazani Shadary, mgombea wa chama tawala na Waziri wa zamani wa mambo ya ndani ambaye amewekewa vikwazo na Umoja wa Ulaya.

Martin Fayulu anawakilisha muungano wa upinzani Lamuka, na anaungwa mkono na Gavana wa zamani wa Katanga Moise Katumbi Chapwe na aliyekuwa Makamu wa rais Jean Pierre Bemba.

Felix Tshisekedi Tshilombo, mtoto wa kiongozi wa zamani wa upinzani Marehemu Ettiene Tshisekedi, anawania kupitia chama kikuu cha UDPS.

 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.