Pata taarifa kuu
DRC-SIASA-USALAMA

Mashine za kupigia kura zaendelea kuzua utata DRC

Mwenyekiti wa tume huru ya Uchaguzi nchini DRCongo (CENI) Corneille Nangaa, amekutana na wagombea kiti cha urais jijini Kinshasa katika mkutano uliodumu saa nne kujadili kuhusu swala la mashine za kupigia kura ambalo limeendelea kuzua utata.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi DRC, Corneille Nangaa.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi DRC, Corneille Nangaa. © JOHN WESSELS / AFP
Matangazo ya kibiashara

Mkutano huo unafanyika wakati wajumbe wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa ukiwasili jijini Kinshasa.

Katika mkutano huo, wagombea wameomba kupewa uthibitisho kuhusu pesa zitakazo fadhili uchaguzi, lakini pia wameendelea kutupilia mbali matumizi ya machine za kupigia kura ambazo zinatarajiwa kutumiwa kwa mara ya kwanza nchini humo katika uchaguzi wa Desemba 23.

Tume huru ya Uchaguzi CENI inasema hakuna njia nyingine mbali na matumizi ya mashine za kupigia kura iwapo kalenda ya uchaguzi wa Desemba 23 inataka kuheshimishwa.

Wagombea kiti cha urais wameendelea kusisitiza pia kuhusu orodha ya watu wanaokadiriwa kuwa asilimia 16,6 ambao hawakutumia mfumo wa kidigitali na ambao upinzani unaona kuwa huenda ni orodha ya watu hewa, jambo ambalo CENI inaona kuwa huo mjadala hauhitajiki maana sheria ya uchaguzi inawapa haki watu ambao hawakutumia mfumo wa kieleketroniki kupigia kura.

Triphon Kinkiey Mulumba ambaye ni mmoja miongoni mwa wagombea anaona kuwa mpaka sasa Tume huru ya Uchaguzi imeshindwa kuweka wazi kuhusu swala la Ufadhili wa uchaguzi.

Katika kutamatisha mkutano huo, Tume Huru ya Uchaguzi na wagombea wote 21 wamekubaliana kuunda tume ya kiufundi kuendelea na majadiliano.

Upande mwingine, mgombea Freddy Matungulu amehoji kuhusu dhamira ya Tume Huru ya Uchaguzi kuandaa mkutano huo siku ambayo wajumbe wa Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa wanawasili jijini Kinshasa.

Katika hatua nyingine mwanamuziki Koffi Olomide ameingia matatani baada ya kutangaza kwamba anapinga matumizi ya mashine za kupigia kura baadhi wakimuunga mkono wengine wakimkashifu kuwa mtu wa kupenda kuzua mkanganyiko baada ya kuwa na kesi za kujibu katika mataifa ya Ufaransa na Zambia.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.