Pata taarifa kuu
MALI-UCHAGUZI-SIASA

Uchaguzi Mali: Ibrahim Boubacar Keïta achaguliwa kwa kura 67.17%

Rais anayemaliza muda wake nchini Mali Ibrahim Boubacar Keïta ("IBK") ameshinda duru ya pili ya uchaguzi wa urais kwa 67.17% ya kura. Mpinzani wake Soumaïla Cissé amepata 32.83% ya kura. Kiwango cha ushiriki kilifikia 34.54%, kulingana na  matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa Alhamisi wiki hii.

Rais anayemaliza muda nchini Mali, Ibrahim Boubacar Keïta atangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais wa Agosti 12 kwa 67.17% ya kura.
Rais anayemaliza muda nchini Mali, Ibrahim Boubacar Keïta atangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais wa Agosti 12 kwa 67.17% ya kura. Michele CATTANI / AFP
Matangazo ya kibiashara

Matokeo hayo ya uchaguzi wa urais wa Agosti 12 yametangazwa na Waziri wa Utawala wa Mali Mohamed Ag Erlaf kwenye radio na televisheni ya taifa. Rais Ibrahim Boubacar Keita ("IBK") ambaye alikua madarakani kwa miaka mitano amechaguliwa ten akuliongoza taifa hilo linalokabiliwa na mdororo wa kiusalama.

Ibrahim Boubacar Keita, maarufu "IBK", ndiye mshindi wa duru ya pili ya uchaguzi, kulingana na matokeo ya awali ya uchaguzi yaliyotangazwa na Waziri wa Utawala. Huu ni ushindi mkubwa kwa sababu amepata 67.17% ya kura. Mpinzani wake, kiongozi wa upinzani Soumaïla Cissé, amepata 32.83% ya kura.

Rais anayemaliza muda wake alipewa nafasi kubwa ya kushinda kabla ya duru ya pili ya uchaguzi. Alishinda kwa karibu asilimia 42 ya kura katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa Julai 31 wakati ambapo alipambana na wagombea wengine 24.

Kwa upande wake, Soumaïla Cissé tayari amekataa matokeo ya uchaguzi, hata kabla ya kutangazwa rasmi kwa matokeo hayo Alhamisi hii, Agosti 16. Amesema uchaguzi wa Agosti 12 uligubikwa na udanganyifu. Jumatano usiku, mkurugenzi wake wa kampeni, Tiébilé Dramé, alionyesha mbele ya vyombo vya habari video inayoonyesha jinsi gani kura zilikua zikiwekwa kinyume cha sheria katika moja ya sanduku za kupigia kura.

Waziri huyo wa zamani wa fedha alijaribu wakati wa kampeni ya uchaguzi kukusanya sauti za upinzani. Soumaïla Cissé alishindwa kupata uungwaji mkono kutoka kwa Cheick Modibo Diarra na Aliou Diallo, ambao mmoja alichukua nafasi ya tatu na mwengine ya nne katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa urais.

Wagombea sasa wana siku chache kuwasilisha madai yao kwa Mahakama ya Katiba. Taasisi hii kuu itathibitisha au la matokeo haya ambayo hadi wakati huu ni ya muda.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.