Pata taarifa kuu
ZIMBABWE-UCHAGUZI-URAIS-UPINZANI

Upinzani nchini Zimbabwe wasema mgombea wake ameshinda urais

Chama kikuu cha upinzani wa nchini Zimbabwe MDC kimetangaza kuwa mgombea wake Nelson Chamisa ndio mshindi wa Uchaguzi wa urais nchini humo.

Nelson Chamisa mgombea Mkuu wa upinzani nchini Zimbabwe
Nelson Chamisa mgombea Mkuu wa upinzani nchini Zimbabwe © AFP
Matangazo ya kibiashara

MDC inaitaka Tume ya Uchaguzi kutangaza mshindi wa Uchaguzi huo, huku kikidai kuwa, chama tawala ZANU PF kinapanga kuiba kura.

Tendai Biti mmoja wa viongozi wa juu nchini humo amewaambia wanahabari jijini Harare kuwa, chama chake kina uhakika wa ushindi lakini wana hofu ya wizi wa kura.

Mapema siku ya Jumanne, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Priscilla Chigumba alisema kuwa hakuna wizi wa kura utakaofanyika na kuongeza kuwa, uamuzi wa wapiga kura ndio utakaoamua mshindi.

Tayari Tume ya Uchaguzi imeanza kutangaza matokeo, huku matokeo ya mwisho yakitarajiwa kufahamika kabla mwisho wa wiki hii.

Awali, rais Emmerson Mnangagwa na kiongozi mkuu wa upinzani Nelson Chamisa, wote wanadai kuwa katika nafasi nzuri ya kushinda Uchaguzi huo.

“Taarifa tunazozipata kutoka kwa wawakilishi wetu, zinaonesha kuwa tunapata ushindi, lakini tunasubiri matokeo kwa mujibu wa Katiba,” amesema Mnangagwa mwenye umri wa miaka 75, kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Naye Chamisa mwenye umri wa miaka 40, amenukuliwa akisema wako tayari kuunda serikali mpya.

“Tunaelekea kupata ushindi mkubwa sana, tumefanya vizuri na tuko tayari kuunda serikali mpya,” amesema Chamisa kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Huu umekuwa ni Uchaguzi wa kwanza, kufanyika bila ya kuwepo kwa rais wa zamani Robert Mugabe ambaye aliondolewa madarakani mwaka 2017, baada ya kuwa madarakani tangu mwaka 1980.

Waangalizi wa kimataifa wameruhusiwa kwenda kutazama Uchaguzi nchini humo kwa mara ya kwanza baada ya miaka 16.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.