Pata taarifa kuu
AFRIKA-VYOMBO VYA HABARI

Chuki dhidi ya wanahabari yaendelea Afrika

Chuki dhidi ya wanahabari na uhuru wa vyombo vya Habari, inaendelea kutishia ukuaji na uimarishwaji wa demokrasia barani Afrika. Burundi, Rwanda, Misri, Somalia, Eritrea na Libya ni miongoni mwa mataifa ambayo wanahabari wanaendelea kufanya kazi kwa uoga.

Demokrasia inaendelea kudidimia kwa sababu ya chuki dhidi ya wanahabari Afrika
Demokrasia inaendelea kudidimia kwa sababu ya chuki dhidi ya wanahabari Afrika Crédit : RSF
Matangazo ya kibiashara

Shirika la Kimataifa la kutetea haki za wanahabari la Maripota wasiokuwa na mipaka, limetaja nchi hizo kutokana na sheria tata zinafanya wanahabari kufanya kazi katika mazingira magumu.

Hata hivyo, Ghana, Afrika Kusini, Burkina Faso, Botswana na Senegal ni baadhi ya mataifa ya Afrika ambayo wanahabari wanashuhudia mazingira mazuri ya kufanya kazi.

Ripoti ya RSF inaeleza kuwa licha ya uhuru kidogo katika nchi hizo, hata hivyo, wanahabari bado wanaogopa kuripoti kwa uwazi kuhusu ripoti za ufisadi zinazowagusa viongozi wa nchi hiyo kwa sababu ya uoga wa kufunguliwa mashtaka.

Wanahabari nchini Burundi, tangu mzozo wa kisiasa na jaribio la mapinduzi dhidi ya rais Pierre Nkurunziza, idadi kubwa wamekimbia nchi hiyo na baadhi ya vituo vikifungwa.

 Jean Bigirimana mwanahabari wa Gazeti la Iwacu hajapatikana tangu kutoweka kwake mwaka 2016 baada ya kuripotiwa kuwa alitoweka baada ya kupokea simu kutoka kwa maafisa wa usalama wa rais Nkurunziza.

Familia na wanahabari wenzake wanaamini kuwa, amezuiwa au kuuawa mikononi mwa maafisa wa usalama.

Nchini Somalia, hali mbaya ya usalama imeendelea kutishia uhuru wa wanahabari kutembea na kuripoti kwa hofu ya kushambuliwa. Mamia wamepoteza maisha katika miaka ya hivi karibuni.

Mataifa ya Afrika Mashariki kama Kenya na Tanzania, hali sio mbaya sana lakini vitendo vya hivi karibuni na serikali za nchi hizo mbili zinaaanza kutishia uhuru wa wanahabari.

Nchini Kenya mwishoni mwa mwezi Januari, serikali kwa karibu wiki moja, ilizima mitambo ya vituo vitatu vya Televisheni, KTN News, Citizen TV na NTV kwa madai kuwa vilipanga kupeperusha kuapishwa kwa kiongozi wa upinzani nchini humo Raila Odinga.

Nchini Tanzania, mwezi Aprili sheria mpya ya mitandao ya kijamii na posta ilipitishwa kuwataka wanahabari wanaomiliki blog na mitandao mingine ya kijamii inayotoa taarifa kusajiliwa na serikali kwa kutoa malipo, suala ambalo linatishia uhuru wa wanahabari nchini humo hasa wale wa kujitegemea.

Pamoja na hilo, kutoweka kwa mwanahabari wa Gazeti la Mwananchi Azory Gwanda aliyekuwa anaandika ripoti za kiusalama katika eneo la Pwani ya nchi hiyo, hajulikani aliko baada ya kutoweka mwaka 2017.

Mbali na changamoto hizo, wanahabari barani Afrika wanakabiliwa na changamoto ya kutolipwa mshahara kwa wakati au hata kutolipwa kabisa, huku ripoti zao zikikataliwa kwa sababu wamiliki wa vyombo vya Habari ni washirika wa karibu wa serikali iliyo madarakani.

Pamoja na hili, ongezeko la Habari za uongo zimeanza kusababisha fani ya uana habari kuanza kupoteza uaminifu kwa sababu ya ripoti zinazochapishwa kupitia mitandoa ya kijamii kama Facebook na Twitter.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.