Pata taarifa kuu
ZIMBABWE-UCHAGUZI-SIASA

Rais wa Zimbabwe atangaza Uchaguzi Mkuu kufanyika "kabla ya mwezi Julai"

Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa ametangaza kwamba Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika mwaka huu nchini Zimbabwe unapaswa kufanyika "kabla ya mwezi Julai". Tangazo hili amelitoa leo Jumatano katika mkutano wa masuala ya kiuchumi unaofanyika Davos, nchini Uswisi.

Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa (kulia), Januari 24, 2018 Davos, Uswisi.
Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa (kulia), Januari 24, 2018 Davos, Uswisi. AFP
Matangazo ya kibiashara

"Mwezi ujao, nitaweza kutangaza tarehe ya uchaguzi, sifikiri kuwa utafanyika mwezi Julai, utafanyika kabla ya mwezi Julai," amesema Rais Mnangagwa, ambaye amemrithi Robert Mugabe mwezi Novemba.

"Wakati huu, uchaguzi wa Zimbabwe utakuwa wa wazi na wenye kuaminika," amesema. "Tunataka uchaguzi huru, wa wazi, na wenye kuaminika ambao hautagubikwa na vurugu," ameeleza Rais Mnangagwa.

Chaguzi zilizotangulia nchini Zimbabwe chini ya zama za Mugabe ziligubigwa na udanganyifu pamoja na vurugu nyingi.

Mnamo mwaka 2008, kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai, aliyeongoza katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa urais, alijiondoa kwenye kinyang'anyiro hicho kwa sababu ya ghasia dhidi ya wafuasi wake.

"Ikiwa tuna vigezo hivyo (vya uwazi na kutokua na vurugu), kwa nini tukatalie waangalizi wa kimataifa kuja katika nchi yetu? Umoja wa Ulaya unakaribishwa," amesema Emmerson Mnangagwa.

"Tunahitaji uchaguzi usio na vurugu. Sisi wanasiasa tunapaswa kuhubiri amani, amani, amani na sio vurugu," amesema.

Mnangagwa alichukua hatamu ya uongozi wa Zimbabwe mnamo mwezi Novemba baada ya kujiuzulu kwa rais Robert Mugabe, akishinikizwa na jeshi, maandamano na na chama chake, Zanu-PF, kumaliza utawala wake wa miaka 37 kama rais wa nchi hiyo.

Makamu wa zamani wa rais na mshirika wa karibu wa Mugabe, Bw Mnangagwa aliteuliwa kupeperusha bendera ya chama cha Zanu-PF katika uchaguzi wa urais. Chama hiki kinaongoza kisiasa nchini Zimbabwe tangu uhuru wa nchi hiyo mnamo mwaka 1980.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.