Pata taarifa kuu
UGANDA-DRC

DRC: Jeshi la Uganda latekeleza mashambulizi dhidi ya kundi la waas wa ADF

Jeshi la Uganda limesema limetekeleza mashambulizi kulenga kambi za waasi mashariki mwa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambako wapiganaji wenye silaha waliwaua wanajeshi 14 wa kulinda amani wa umoja wa Mataifa.

Wanajeshi wa DRC wakiwa kwenye moja ya misitu ambayo wanaamini waasi wa ADF wanajificha
Wanajeshi wa DRC wakiwa kwenye moja ya misitu ambayo wanaamini waasi wa ADF wanajificha RFI/Sonia Rolley
Matangazo ya kibiashara

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na jeshi la Uganda imesema kuwa baada ya kubadilishana taarifa za kiintelijensia kati yake na Serikali ya DRC walibaini mpango wa waasi wa ADF ambao hivi karibuni walishambulia kambi ya walinda amani, kuwa walikuwa wanapanga kutatiza usalama nchini Uganda.

Kwa mujibu wa umoja wa Mataifa waasi wa Uganda wa ADF ambao wengine ni waislamu wenye msimamo kali ndio waliohusika na shambulizi na kuua walinda amani 14 wa Tanzania wiki mbili zilizopita.

Kundi la ADF lilianza kwa kujaribu kumpindua rais wa Uganda Yoweri Museveni ambaye walidai ni tishio kwa Waislamu lakini hata hivyo likajiunga na makundi mengine na kuanza kutekeleza mashambulizi mwaka 1995.

Baada ya kufurushwa na majeshi ya Uganda magharibi mwa nchi hiyo, kundi la ADF lilihamishia shughuli zake mashariki mwa nchi ya DRC.

Kundi hili pia linalaumiwa kwa shambulio dhidi ya walinda amani wa tume ya MONUSCO mwezi Octoba mwaka huu ambapo walinda amani wawili waliuawa na wengine 12 kujeruhiwa.

Kundi hili linatuhumiwa na Serikali ya DRC pamoja na tume ya umoja wa Mataifa nchini DRC MONUSCO kwa kuhusika na mauaji ya watu zaidi ya 700 mjini Beni tangu mwezi Octoba mwaka 2014.

Wapiganaji wengi kutoka kwenye kundi hili wanadaiwa kusajiliwa kutoka nchini Tanzania, Burundi, Kenya na hata ndani ya Somalia.

Ripoti mbalimbali zinaonesha kuwa kundi hilo linashirikiana pia na baadhi ya wanajeshi wa Serikali ya DRC katika kutekeleza mauaji mashariki mwa nchi hiyo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.