Pata taarifa kuu
ANC-AFRIKA KUSINI

Ramaphosa achaguliwa kuwa kiongozi mpya wa chama cha ANC

Chama tawala nchini Afrika Kusini ANC kimemchagua Cyril Ramaphosa kumrithi rais Jacob Zuma kama kiongozi wa chama katika uchaguzi uliokuwa na ushindani na mvutano mkubwa wa namna zoezi la upigaji kura lilivyofanyika.

Makamu wa rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ambaye sasa anakuwa kiongozi mpya wa chama akipongezwa baada ya kutangazwa mshindi. 18 Desemba 2017.
Makamu wa rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ambaye sasa anakuwa kiongozi mpya wa chama akipongezwa baada ya kutangazwa mshindi. 18 Desemba 2017. REUTERS/Siphiwe Sibeko
Matangazo ya kibiashara

Makamu wa rais Ramaphosa amemshinda mpinzani wake wa karibu ambaye aliwahi kuwa waziri na baadae mkuu wa tume ya umoja wa Afrika Nkosazana Dlamin-Zuma ambaye pia aliwahi kuwa mke wa rais Zuma.

Kwa matokeo haya sasa yanamfanya makamu wa rais Cyril Ramaphosa kuwa kwenye nafasi nzuri ya kushinda kiti cha urais wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2019.

Mivutano ya kisiasa ndani ya chama ilisababisha sintofahamu kubwa na hofu kuwa huenda chama kingegawanyika hata kabla ya zoezi lenyewe la uchaguzi.

Ramaphosa amemshinda Dlamini-Zuma kwa kura 2440 dhidi ya kura 2261 alizozipata mpinzani wake.

Matokeo yaliyompa ushindi Ramaphosa yalisababisha hata wajumbe wa juu wa chama tawala kuamka na kushangilia kwa furaha ndani ya ukumbi na kwenye mitaa ya jiji la Johannesburg.

Ramaphosa mwenye umri wa miaka 65 amekuwa akizungumza kwa ukali kuhusu masuala ya rushwa ndani ya chama na Serikali vitendo vilivyokuwa vikifadhiliwa na wafanyabiashara wakubwa.

Kiongozi huyu alipiga kampeni zake kwa kumkosoa mtangulizi wake rais Zuma na kuapa kuwashughulikia watuhumiwa wa masuala ya ufisadi na ushindi wake huenda ukataka kumuitisha rais Zuma kwenye baraza la chama kumjadili juma lijalo.

Chama cha ANC kilimuita aliyekuwa rais wakati huo Thabo Mbeki mwaka 2008 baada ya rais Zuma kuchaguliwa kuwa kiongozi wa chama ambapo baadae walimvua madaraka ndani ya chama na kumlazimisha ajiuzulu nafasi yake.

Wadadisi wa mambo wanaona kuwa kilichomtokea Thabo Mbeki huenda kikamtokea rais Zuma ikiwa kiongozi mpya wa chama Ramaphosa ataamua kumuita kwenye baraza la ANC kumuhoji kutokana na tuhuma zinazomkabili.

Kwa miezi kadhaa rais Zuma amekuwa akikabiliwa na kesi mbalimbali za ufisadi huku nyingi zikimuhusisha kupokea rushwa kutoka kwa familia za wafanayabiashara wa kihindi nchini Afrika Kusini.

Mpaka sasa mustakabali wa rais Zuma bado uko mashakani.

Ramaphosa ametokea wapi:

Alizaliwa mjini Soweto, Johannesburg mwaka 1952, aliwahi kukamatwa na kufungwa kwenye miaka ya 1974 hadi 1976 kutokana na harakati zake za kupinga ubaguzi wa rangi. Ndiye pia alikuwa muanzilishi wa chama cha wafanyakazi wa migodini NUM mwaka 1982.

Mwaka 1990 alikuwa kwenye kamati maalumu ya kitaifa ilihusika katika maandalizi ya kuhakikisha rais wa kwanza mweusi wa nchi hiyo marehemu Nelson Mandela anaachiliwa kutoka jela.

Mwaka 1994 alichaguliwa kuwa mbunge katika bunge la kitaifa. Na baadae mwaka 1977 aliachana na siasa na kuamua kuwa mfanyabiashara, ambapo alikuwa miongoni mwa wafanyabiashara matajiri nchini Afrika Kusini.

Alikuwa kwenye kamati iliyochunguza mauaji ya wafanyakazi wa mgodini kule Marikana mwaka 2012 na kisha baadae akachaguliwa kuwa rmakamu wa rais mwaka 2014.

Na tarehe 18 ya mwezi Desemba mwaka 2017 anachaguliwa kuwa kiongozi wa chama tawala cha ANC na mgombea katika uchaguzi mkuu wa urais utakaofanyika.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.