Pata taarifa kuu
TANZANIA-KODI

Wataalamu: Kudhibiti wakwepaji kodi kunahitaji juhudi za kimataifa

Wataalamu wa masuala ya uchumi na kodi wameonya kuhusu uwezekano wa dunia kuendelea kushuhudia kuongezeka kwa vitendo vya ukwepaji kodi na ufichaji wa mitaji kwenye mataifa ambayo hayana mifumo ya udhibiti wa kodi au hayatozi kodi kabisa.

Balozi wa Norway nchini Tanzania, Hanne-Marie Kaastard akizungumza wakati wa uzinduzi wa kitabu kinachohusu kodi za kimataifa. 30 Novemba 2017
Balozi wa Norway nchini Tanzania, Hanne-Marie Kaastard akizungumza wakati wa uzinduzi wa kitabu kinachohusu kodi za kimataifa. 30 Novemba 2017 NgowiTV
Matangazo ya kibiashara

Haya yamesemwa hii leo jijini Dar es Salaam, wakati wa uzinduzi wa kitabu kinachohusu kodi za kimataifa na mtiririko wa mitaji kutoka barani Afrika, kitabu ambacho ni sehemu ya mradi unaofadhiliwa na taasisi ya utafiti ya nchini Norway na ambao umehusisha nchi za Tanzania, Zambia na Angola.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, balozi wa Norway nchini Tanzania Hanne-Marie Kaastard, amesema vita dhidi ya watu na makampuni yanayokwepa kodi inapaswa kuwa vita ya kimataifa na kwamba wanasiasa pekee hawawezi kuimaliza ikiwa wananchi hawatashirikishwa.

“Ili wanasiasa wachukue hatua na kulizungujmzia suala hili! Uelewa unahitajika, kwa sababu suala hili sio la wanasiasa peke yake! Ukweli ni kwamba hili ni suala la kila mwananchi”.

Kwa upande wake mtaalamu wa masuala ya kodi kutoka taasisi ya utafiti ya Norway na mhadhiri katika chuo kikuu cha kodi cha Afrika kilichoko mjini Pretoria Afrika Kusini, Profesa Odd-Helge Fiestard, amesema kadiri siku zinavyozidi kwenda vita hii inakuwa ngumu na kwamba madhara yale nchi zinazoendelea zinashindwa kupata mapato stahiki ambayo yangetumika kuwaletea maendeleo wananchi.

“Serikali zinapoteza mapato mengi sana ambayo yangeweza kutumika kuleta maendeleo kwa uma, hili linaathiri pia namna ya mgawanyo wa kipato kwa sababu ya hao matajiri wanaotengeneza mfumo unaosababisha kuongezeka kwa ombwe la walionacho na wasionacho”.

Profesa Odd ameongeza kuwa ili kudhibiti suala hili taasisi muhimu kama ile ya umoja wa Afrika na kitengo cha kodi cha umoja wa Mataifa zinapaswa kufanya kazi kwa pamoja na kwa ukaribu.

Licha ya ripoti mbalimbali za uchunguzi kuonesha namna mashirika makubwa ya kimataifa na hata viongozi wa dunia wanaoficha fedha zao kwenye nchi ambazo hazitozi kodi, bado mataifa yamegawanyika kuhusu hatua za kuchukua.

Kwa upande wake Profesa Honesty Ngowi mtaalamu wa masuala ya uchumi na mhadhiri katika chuo kikuu cha Mzumbe tawi la dar es Salaam, nchini Tanzania, anasema suala la ukwepaji kodi linaathiri maendeleo ya nchi kwa kuwa inapoteza mapato mengi ambayo yangeweza kutokana na ulipaji kodi zilizo sahihi.

Profesa Ngowi amesema baadhi ya nchi zimekuwa na mifumo ya kifedha na kodi ambayo sio rafiki na hivyo kutengeneza mianya ambayo watu na makampuni haya makubwa yamekuwa yakiutumia kukwepa kodi.

“Suala la ukwepaji kodi ni la kimataifa na linahitaji juhudi za kimataifa na hasa kwa mataifa ambayo yanafahamika kuwa kotivu cha watu kuficha fedha basi zitoe ushirikiano, vinginevyo hakuan kitu kitakachowezekana katika kuweka udhibiti”.

Ukwepaji kodi na uhamishaji wa mitaji kutoka mataifa ya Afrika kunakofanywa na makampuni makubwa kumeendelea kulifanya bara hili kuwa masikini licha ya rasilimali ilizonazo, na sasa wataalamu wanahofia kuwa huenda hali ikawa mbaya zaidi ikiwa jitihada za pamoja hazitachukuliwa kudhibiti hali hii.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.