Pata taarifa kuu
ZIMBABWE-SIASA-AFRIKA

Emmerson Mnangagwa aapishwa kuwa rais mpya wa Zimbabwe

Emmerson Mnangagwa, ameapishwa kuwa rais mpya wa Zimbabwe mbele ya maelfu ya raia wa nchi hiyo. Mnangagwa, anakuwa rais wa pili wa taifa hilo la Kusini mwa Afrika lililopata uhuru wake mwaka 1980.

Emmerson Mnangagwa rais mpya wa Zimbabwe akiapishwa jijini Harare
Emmerson Mnangagwa rais mpya wa Zimbabwe akiapishwa jijini Harare REUTERS
Matangazo ya kibiashara

Hatua hii imekuja baada ya kujiuzulu kwa rais wa zamani Robert Mugabe wiki hii baada ya kuongoza nchi hiyo kwa miaka 37.

“ Mimi Emmerson Dambudzo Mnangagwa naapa kuwa rais wa Zimbabwe. Nitakuwa mwaminifu na kutii na kuilinda Katiba ya nchi,” alisema huku akishangiliwa.

Mnangagwa ameshangaliwa na maelfu ya raia wa nchi hiyo waliofika kushuhudia mabadiliko ya uongozini nchini humo.

Mbali na raia wa Zimbabwe, viongozi wengine wa Afrika wanashuhudia mabadiliko hayo akiwemo rais wa Zambia Edgar Lungu na Ian Khama wa Bostwana.

Rais wa zamani Zambia Keneth Kaunda na Rupia Banda nao pia wanahudhuria sherehe hizo jijini Harare.

Rais wa zamani Robert Mugabe hajaonekana katika sherehe hizo za kihistoria.

Katika hotuba yake, Mnangagwa amesema atakuwa rais wa wananchi wote wa Zimbabwe.

Aidha, ameahidi kuimarisha uchumi wa nchi hiyo na kuunda nafasi za kazi hasa kwa vijana.

Pamoja na hilo, rais Mnangagwa ameyaomba mataifa yaliyoiwekea nchi hiyo vikwazo vya kiuchumi kuondoa vikwazo hivyo na kuisaidia kuimarika zaidi kiuchumi.

"Hakuna taifa lolote linaloweza kusimama peke yake, dunia imekuwa kama kijiji na hakuna anayeweza kusimama peke yake," amesema.

Rais huyo mpya, amewahakikishia wawekezaji wa kigeni kuwa uwekezaji wao utakuwa salama nchini humo.

Ameahidi pia Uchaguzi Mkuu utafanyika mwaka ujao kama ilivyopangwa.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.