Pata taarifa kuu
TANZANIA

Rais Magufuli ateua waziri mpya wa Madini na Nishati, abadili baraza lake la mawaziri

Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli amemteua waziri mpya wa Nishati na Madini huku akiongeza idadi ya wizara katika baraza lake jipya la mawaziri alilolitangaza Jumamosi ya Octoba 7.

Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli, akizungumza wakati akitangaza kufanya mabadiliko ya baraza lake la mawaziri. 7 Octoba 2017
Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli, akizungumza wakati akitangaza kufanya mabadiliko ya baraza lake la mawaziri. 7 Octoba 2017 Ikulu/Tanzania
Matangazo ya kibiashara

Katika mabadiliko hayo Rais Magufuli ameongeza idadi ya Wizara na Mawaziri wake kutoka 19 hadi 21, na Naibu Mawaziri kutoka 16 hadi 21.

Kwa sasa iliyokuwa wizara ya Nishati na Madini imegawanywa ambapo kutakuwa na wizara ya Nishati inayojitegemea na wizara ya Madini inayojitegemea. Wizara nyingine zilizogawanywa ni pamoja na iliyokuwa wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambayo sasa kutakuwa na wizara ya Kilimo na wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Wizara ya Nishati na Madini imegawanywa ikiwa ni miezi michache tu imepita toka amfute kazi aliyekuwa waziri wake wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo baada ya kupokea ripoti ilioonesha kulikuwa na uzembe wa kuingiwa kwa mikataba ya madini nchini humo.

Wizara ya Nishati na Madini ni miongoni mwa wizara ngumu zaidi kuongoza nchini Tanzania ambapo hata wakati wa utawala wa awamu ya nne, wizara hiyo ilishwahi kufanyiwa mabadiliko kadhaa ya mawaziri.

Wadadisi wa mambo wanaona kuwa uamuzi huu wa rais Magufuli kutenganisha Nishati na Madini, kumetokana na hatua alizotangaza kuzichukua hivi karibuni kuhusu sekta ya Madini na Nishati.

Toka mwanzoni mwa mwaka huu rais Magufuli aliagiza kutosafirishwa kwenda nje ya nchi mchanga wa dhahabu ambapo aliagiza kuundwa kwa tume kuchunguza mchanga huo, huku hivi karibuni kamati ya bunge ikimkabidhi ripoti kuhusu biashara ya Tanzanite na Almasi ambako nako kulibainika kuwepo kwa dosari nyingi za kimikataba.

Rais Magufuli amekuwa awashutumu baadhi ya viongozi waliotangulia pamoja na wawekezaji kwa kuisababishia nchi yake hasara kutokana na kufanya biashara ambayo haikuwa na faida kwa nchi ya Tanzania.

Rais Magufuli sasa amemteua Medard Kalemani kuwa waziri wa Nishati huku wizara ya Madini akimteua aliyekuwa waziri wa Utumishi Angellah Kairuki.

Wizara nyingine zilizofanyiwa mabadiliko ni pamoja na wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na ile ya Kilimo na Mifugo na Uvuvi.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.