WFP: Hatuna fedha za kukidhi mahitaji ya walengwa Nigeria
Shirika la Mpango wa chakula duniani WFP linasema limekabiliwa na uhaba wa fedha, itaweza tu kutoa msaada kwa watu 400,000 waliokimbia makwao Kaskazini mwa Nigeria kutokana na tishio la kundi la kigaidi la Boko Haram.
Imechapishwa:
WFP inasema ilikuwa imepanga kuwafikia watu Milioni 1 nukta 8 mwaka huu lakini ukosefu wa fedha umewalazimisha kubadilisha mipango yao.
Umoja wa Mataifa unasema unahitaji Dola za Marekani Bilioni 1.05 kuwasaidia watu hao.
Wakati huo huo wapiganaji wa Boko Haram wamefanya mashambilizi makali katika mji ulioko kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Watu walioshuhudia wanasema mashambulizi hayo makali yametokea wakati waislamu wakijiandaa kufuturu katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhan.
Picha ya video ambayo haijathibitishwa iliyotumwa katika mtandao wa Twitter inaonesha wanawake na watoto wakikimbia kutokana na mashambulizi hayo.
Wapiganaji wa Boko Haram wameteketeza eneo la kaskazini mashariki mwa Nigeria kwa kuua maelfu ya watu na kulazimisha wengine milioni mbili kuyakimbia makaazi yao.