Pata taarifa kuu
GAMBIA-SENEGAL-AU

Rais mpya wa Gambia, Adama Barrow aapishwa nchini Senegal

Rais mteule wa Gambia, Adama Barrow, hatimaye ameapishwa rasmi kuwa rais wa nchi hiyo katika ofisi za ubalozi wa Gambia zilizoko jijini Dakar, Senegal, huku akitoa wito kwa wanajeshi kuonesha utii kwa Serikali yake.

Adama Barrow, wakati wa kuapishwa kwake katika ofisi za ubalozi wa Gambia mjini Dakar, nchini Senegal, Januari 19, 2017.
Adama Barrow, wakati wa kuapishwa kwake katika ofisi za ubalozi wa Gambia mjini Dakar, nchini Senegal, Januari 19, 2017. SENEGALESE PRESIDENCY / AFP
Matangazo ya kibiashara

Rais Barrow, amelazimika kuapishwa nje ya nchi yake kutokana na kuhofia usalama wake pamoja na hatua ya rais Yahya Jammeh kukataa kuondoka madarakani, akipinga matokeo ya uchaguzi wa mwezi Desemba mwaka jana.

Awali kabla ya kuapishwa kwake, wizara ya mambo ya nje ya Senegal ilidai kuwa kiongozi huyo angeapishwa kwenye ardhi ya nchi yake, lakini haikuwa hivyo na sasa rais Barrow amekula kiapo cha utii kwa nchi yake kwenye ubalozi wa Gambia nchini Senegal.

Barrow toka kutangazwa kuwa mshindi wa kiti cha urais, ameungwa mkono na Jumuiya ya Kimataifa, lakini mpinzani wake Yahya Jammeh amekataa kuondoka madarakani, akitaka kwanza pingamizi lake la uchaguzi lisikilizwe na mahakama kuu iliyosema inauwezo wa kusikiliza shauri hilo mwezi May.

Viongozi wa nchi za Afrika Magharibi wamejaribu kumshawishi rais Jammeh kuondoka madarakani bila mafanikio na kutishia kumuondoa kwa kutumia nguvu za kijeshi.

Yahya Jammeh, aliyekuwa rais wa Gambia ambaye ameng'ang'ania madarakani
Yahya Jammeh, aliyekuwa rais wa Gambia ambaye ameng'ang'ania madarakani MARCO LONGARI / AFP

Mabalizo wa nchi za kigeni wanaoziwakilisha nchi zao nchini Senegal, walishiriki kwenye sherehe za kuapishwa rais Barrow, huku maelfu ya raia wa Gambia wanaoishi nchini Senegal wakiwa wamefurika nje ya ubalozi wa nchi yao jijini Dakar kushuhudia sherehe hizo.

Katika hatua nyingine pendekezo la nchi ya Senegal kwa baraza la usalama lililotaka nchi wanachama kuunga mkono juhudi za ECOWAS, huenda hata likipitishwa lisiwe na nguvu sana, kwakuwa tayari rais Barrow ameomba usaidizi wa jumuiya ya kimataifa kumsaidia kuleta usalama na amani nchini mwake.

Haijulikani ikiwa mataifa ya nchi za Afrika Magharibi yatatumia nguvu kumuondoa Jammeh madarakani, au nguvu ya diplomasia itatumika kumshawishi aondoke mwenyewe kwa hiari.

Nchi kadhaa za Afrika zilijitolea kumpa hifadhi rais Jammeh ikiwa angeondoka mwenyewe kwa hiari.

Vikosi vya nchi ya Senegal na Ghana tayari viko kwenye mpaka na nchi ya Gambia, na tayari ndege za Nigeria zimeripotiwa kupiga doria kwenye anga la nchi ya Gambia.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.