Pata taarifa kuu
GAMBIA

Gambia: Rais Jammeh atangaza hali ya hatari siku 2 kabla ya kuapishwa kwa Adama Barrow

Rais wa Gambia, Yahya Jammeh Jumanne ya wiki hii ametangaza hali ya hatari nchini mwake, akidai uchaguzi mkuu wa mwaka jana alioshindwa dhidi ya mpinzani wake Adama Barrow, uliingiliwa na nchi za kigeni.

Rais wa Gambia, Yahya Jammeh, hii ni picha ya kumbukumbu akiwa nchini Morocco mwaka 2014
Rais wa Gambia, Yahya Jammeh, hii ni picha ya kumbukumbu akiwa nchini Morocco mwaka 2014 ISSOUF SANOGO / AFP
Matangazo ya kibiashara

Rais Jammeh amesema kuwa "tangazo hili lilikuwa ni muhimu kutokana na kuingiliwa kwa kiwango cha juu kwa uchaguzi mkuu wa Desemba mosi mwaka jana na pia kuingiliwa kwa masuala ya ndani ya Gambia," amesema Jammeh kupitia tangazo la televisheni.

Kiongozi huyo ameongeza kuwa "hatua hii imesababisha kutengeneza mazingira ya hofu, na kutishia uhuru wake, amani na usalama," aliongeza Jammeh.

Kwa mujibu wa katiba ya Gambia, ikiwa rais ndio ametangaza hali ya hatari, kisheria hali hiyo itadumu kwa siku saba, na itadumu kwa siku 90 ikiwa bunge la nchi hiyo litapitisha.

Tangazo la rais Jammeh amelitoa wakati zikiwa zimesalia siku mbili tu, kabla ya kufanyika kwa sherehe za kuapishwa kwa rais mteule, Adama Barrow ambaye alipata ushindi mkubwa kwenye uchaguzi wa mwaka jana.

Rais mteule wa Gambia, Adama Barrow, ambaye anasubiri kuapishwa. 2016
Rais mteule wa Gambia, Adama Barrow, ambaye anasubiri kuapishwa. 2016 REUTERS/ Thierry Gouegno

Tayari rais Jammeh amekataa kushindwa kwenye uchaguzi huo, na alishatangaza kuwa hatoondoka madarakani ifikapo Januari 19 mwaka huu kama anavyotakiwa kwa mujibu wa katiba, kuwa amekabidhi madaraka kwa rais mteule.

Rais Jammeh amesema hawezi kuondoka madarakani hadi pale mahakama ya juu nchini humo itakaposikiliza shauri lake la kupinga matokeo, alilowasilisha siku chache baada ya kukataa matokeo, ambapo hakukuwa na majaji wa kutosha kusikiliza shauri hilo na kusogezwa hadi mwezi May.

Kwa sasa rais mteule Adama Barrow, anapatiwa hifadhi nchini Senegal, na nchik hiyo ilisema ingemsafirisha kwenda nchini humo siku ya Alhamisi kwaajili ya sherehe za kuapishwa.

Nchi za jumuiya ya ECOWAS tayari zimemuonya rais Jammeh, kuwa zitatumia nguvu za kijeshi kumuondoa madarakani ikiwa yeye mwenyewe hata ondoka kwa hiari.

Taarifa zinasema kuwa, meli za kivita za Senegal tayari zimesogea kwenye pwani ya bahari ya Gambia, katika kile kinachoonekana uwepo wa uwezekano mkubwa wa kutumika kwa nguvu za kijeshi kumuondoa rais Jammeh.

Umoja wa Mataifa pia umetaka kuwepo kwa mabadilishano ya amani ya madaraka kati ya rais Jammeh na rais mteule Adama Barrow.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.