Pata taarifa kuu
GAMBIA-SIASA

Wasuluhishi wa ECOWAS wakutana kujadili hatima ya rais Yahya Jammeh

Wasuluhishi wa mzozo wa kisiasa nchini Gambia kutoka muungano wa kiuchumi wa nchi za Afrika Magharibi ECOWAS, wanakutana jijini Abuja nchini Nigeria, kujadili hatima ya rais Yahya Jammeh ambaye amekataa kuondoka madarakani baada ya kushindwa katika Uchaguzi wa mwezi Desemba mwaka uliopita dhidi ya mpinzani wake Adama Barrow.

Rais  Yahya Jammeh alipokutana na ujumbe wa ECOWAS tarehe 13 Desemba 2016 jijini Banjul
Rais Yahya Jammeh alipokutana na ujumbe wa ECOWAS tarehe 13 Desemba 2016 jijini Banjul REUTERS/Stringer
Matangazo ya kibiashara

Mwenyekiti wa ECOWAS Ellen Johnson Sirleaf ambaye pia ni rais wa Liberia, mwishoni mwa wiki iliyopita akiwa jijini Accra nchini Ghana, alisema muungano huo unafuatilia kwa karibu kinachofanyika nchini Gambia, na muungano huo utahakikisha kuwa uamuzi wa raia wa Gambia unaheshimiwa.

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari ambaye anaongoza ujumbe wa wasuluhishi hao, anatarajiwa kutoa mwelekeo wa namna mazungumzo yatakavyokuwa yamefikia baadaye siku ya Jumatatu.

Haya yote yanakuja wakati huu Mahakama ya Juu ikitarajiwa kuanza kusikiliza kesi iliyowasilishwa na rais Jammeh, kutaka uchaguzi huo kufutwa kwa madai kuwa  Barrow aliyetangazwa mshindi, hakushinda kihalali.

Uamuzi kuhusu mgogoro huu wa Gambia, unastahili kufanyika kufikia tarehe 19 mwezi huu siku ya mwisho ya utawala wa rais Jammeh ambaye ameongoza nchi hiyo kwa miaka 22.

Ripoti zinasema kuwa, huenda jeshi la Senegal likaingilia kati na kumwondoa kwa nguvu rais Jammeh ikiwa atakataa kabisa kuondoka madarakani.

Wakati uo huo, serikali ya Gambia imekifungia kituo kingine cha redio, Paradise FM bila ya kutoa maelezo yoyote.

Hii ndio redio ya nne kufungwa nchini humo na watu wanaosema ni maafisa wa usalama, waliopewa maagizo kufanya hivyo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.